SciDev.Net

Pages

Thursday, July 22, 2010



RAS MKUMBUU PEMBA

RAS MKUMBUU YAPATA MRADI WA HIFADHI YA MAZINGIRA YA BAHARI

Na Ali Haji Hamad, Pemba Press Club
Eneo la bahari ya Ras Mkumbuu Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini- Pemba. Limechaguliwa kuwa mojawapo ya maeneo mawili ya Tanzania yatayoanzishwa mradi wa mfano (demonstration project) wa Uhifadhi wa Mazingira ya bahari na uendelezaji wa jamii iliyozunguka kupitia mradi mkubwa wa uhifadhi wa mazingira ya Bahari unaojulikana kwa jina Agulhas and Somali Current Large Marine Ecosystem Project (ASCLME)

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika tovuti ya Mradi huo, (www.dlist-asclme.org) utaofadhiliwa na Global Environmeantal Facility (GEF) na kutekelezwa na shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) mbali na eneo la Ras Mkumbuu – kisiwani Pemba eneo jengine la Tanzania ambalo limo kweneye mradi huo ni eneo la Kilwa Tanzania Bara.

Pamojana Tanzania Mradi wa ASCLME utaendeshwa pia katika nchi nyengine nane zikiwemo Afrika Kusini, Somalia, Kenya, Msumbiji, Madagasca, Mauritaus, Comoro na Seychelles kwamuda wa miaka mitano kwa gharamaza zaidi ya shilingi za Tanzania Bilioni 17 (US$ 12.2milioni)

Kwa mujibu wa tovuti ya mradi wa ASCLME eneo la Ras Mkumbuu ambalo lipokaribu kabisa na eneola hifadhi ya kisiwa cha Misali –Pemba limechaguliwa kutokana na kuwa kwake katika nafasi nzuri ya ki-jeografia na kuwa na utajiri wa matumbawe, aina mbalimbali za samaki na rasilimali ya viumbe vidogovidogo vya bahari ambavyo viko hatarini kuathiriwa bila kuwepo na mikakati ya uhifadhi.

Katika kuhakisha ushiriki wa wananchi wenyeji katika utekelezaji wa mradi huo na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari tayari kazi za kuwajumuisha wananchi wa vijiji vy karibu na Ras Mkumbuu katika mipango ya utekelezaji zimeanza kwa kusikiliza maoni ya wanachi juu yamiradi wanayopenda ianzishwe ili kuwasaidia kuboresha huduma za kijamii, kukuza uchumi na kupunguza shindikizo kwa matumizi ya rasilimali za bahari.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Meneja wa Taasisi ya EcoAfrica Environmental Consultants (Tanzania) - Frida Lanshammar ambayo ndiyo iliyohusika na upembuzi yakinifu wa mradi ASCLME alifanya ziara katika Vijiji vilivyo jirani vya Wesha Shehia ya Wesha na Ndagoni, Shehia ya Ndagoni Wilaya y a Chake Chake kujadiliana na wananchi wa huko juu ya jinsi wananvyo weza kufaidika na mradi huo.

Meneja huyo alisema wananchi wa vijiji hivyo kupitia kamati zao za maendeleo wamechagua kuanzishiwa vituo viwili vikubwa vya maendeleo ya kijamii(kimoja katika kila shehia) vitakavyojumuisha ndani yake huduma muhimu za kijamii na kiuchumi zinazohitajiwa na wanaanchi wa hapo.

Meneja Frida amezitaja baadhi ya huduma ambazo zimebainishwa na wanachi wa huko kama vipaumbele vinavyotakiwa kuwemo katika vituo hivyo vya maendeleo ya kijamii kuwa ni huduma za kumbi za mikutano, ofisi ya shughuli za kitalii, darasa la kisomo cha watu wazima, chumba cha computer na Internet. Huduma nyengine ni soko la kuuzia mboga mboga na matunda, sehemu yakukaushia mazao ya baharini na matunda, vyoo na sehemu maalum kwaajili ya huduma ya Afya.

Frida amesema hata hivyo bado ni mapema mno kuzungumzia gharama halisi za ujenzi wa vituo hivyo ambavyo ufadhili wake utakuwa nje ya mradi mkubwa na iwapo ujenzi wake utajumuisha kila kitu ambacho wananchi wa vijiji hivyo wamechaguwa kujumuishwa kwa vile itategemea zaidi mhisani ataejitokeza kuufadhili ujenzi wa vituo hivyo vya kijamii.

Hata hivyo katika hatua za awali tayari shirika la maendeleo la Denmark DANIDA limeonesha nia ya kufadhili ujenzi wa vituo hivyo na tayari kwa kuanzia limekuwa mstari wa mbele katika kugharamia mchakato mzima wa kupata maoni ya wananchi juu vituo vya maendeleo ya kijamii na kusaidia pia upatikanaji wa michoro ya ujenzi .

Katika ziara ya hivi karibuni ambayo ilifadhiliwa pia na shirika la maendeleo la Denmark DANIDA wananchi wa vijiji vya Ndagoni na Wesha walifanikiwa kushirikiana na Mtaalamu wa Michoro na Usanifu majenzi kutoka Afrika Kusini Profesa K. Barker kuchaguwa maeneo ya Skuli ya Wesha na Skuli ya Ndagoni kuwa yanaweza kutumika kujenga vituo hivyo vya kijamii

Sheha Kahatan, mkaazi wa Shehia ya Ndagoni na mjumbe wakamati ya maendeleo ya shehia hiyo amesema kuwepo kwa vituo vya aina hiyo imekuwa ni ndoto yao ya siku nyingi na kupatikana kwa fursa hiyo kutawasaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na umasikini wa kipato na kuimarika kwa huduma za kijamii kijijini kwao.

Mwanakijiji huyo amesema wao kilio chao kikubwa katika shehia ya Ndagoni ni kupatikana kwa huduma za afya katika kituo hicho na kuwaondoshea tatizo la sasa ambapo wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita nne hadi kituo cha Afya cha Wesha kufuata hata huduma ndogo tu za kufunga vidonda.

MWISHO

MARPS Zanzibar

VIONGOZI WA DINI WAAHIDI KUSAIDIA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA HIV MIONGONI MWA MARPS ZANZIBAR
Na Ali Haji Hamad, Pemba Press Club
Viongozi wa dini wameahidi kila mmoja kwa nafasi yake kuendelezeza jitihada za kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU na UKIMWI miongoni mwa makundi hatarishi (MARPS) Zanzibar.
Wakizungumza katika mkutano wa kutathmini Utendaji wa jumuiya ya taasisi za kidini ya Maendeleo na Mapambano ya Ukimwi Zanzibar (ZIADA) wanadini hao wamesema japo matendo yanayofanywa na kundi hilo ambalo linajumuisha watumiaji wa madawa ya kulevya, wanaume wanaufanya mapenzi na wanaume wenzao (mashoga) na wafanyaji wa biashara ya ukahaba hayakubaliki katika dini hizo lakini bado viongozi wa dini wanawajibu wa kuwanusuru na kuwaelekeza katika mwenendo unaokubalika.
“Tusiwatenge tuwaweke karibu, tuwaelekeze madhara ya matendo wanayoyafanya kwa maisha yao ya dunia na maisha yao ya baadae akhera nadhani hiyo ndiyo njia bora ya kuyasaidia makundi haya hatarishi” alisema bi Bi Ramla Salim wa Skuli ya Kiislamu Kizimbani alipokuwa akichangia mjadala huo.
Naye ustadhi Muhammed Massoud Said wa msikiti wa Vijana Wete alielezea kusikitishwa kwake na tabia ya viongozi wa dini ya kuyapuuza moja kwa moja makundi hayo kama vile wao si sehemu ya jamii. “Tumekuwa tukiyapuuza makundi hayo, hatutaki kuonana nao, kuzungumza nao wala kuwafikia katika harakati zetu tunazofanya, hata tukikutana nao barabarani kwa bahati mbaya tunageuza uso tusiwaone.
Hili si jambo jema na nadhani tukifanya hivi tutakuwa bado hatujawasidia” alsema ustadhi Muhammed Akielezea ubaya wa kuyapuuza makundi hayo ustadhi Muhammed alisema yakiendelea kuachwa bila kufanyiwa mkakati wa kuyasaidia, matendo mabaya wanayoyafanya yanaweza kukua na kutapakaa na madhara yake kuingia katika jamii nzima kwa vile bado makundi hayo ni sehemu ya jamii ya Wazanzibari na maisha yao ya kila siku yana mwingiliano wa moja kwa moja na maisha ya watu wengine wa kawaida.
Hata hivyo baadhi ya viongozi waliohudhuria walielezea wasi wasi wao kuhusu jinsi ya kuyafikia makundi hatarishi kwa vile njia zinazotumiwa sasa na viongozi wa dini kutowa elimu ya VVU na UKIMWI kama vile hotuba katika sala za Ijumaa, mihadhara na madrassa haziwagusi moja kwa moja watu hao.
“Jambo moja la kukumbuka ni kwamba hapa tunazungumzia watumiaji wa madawa ya kulevya, wafanyaji wa biashara ya ukahaba na mashoga na hawa hawahudhirii misikitini, hawajitokeze kwenye mawaidha wala hawaendi Madrassa jee tutatumia njia gani ili kwafikia” alitoa changamoto Dr. Issa Ziddi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Utafititi wa Integrated Behavioral and Biological Surveillance Survey (IBBSS) uliofanywa na Kitengo cha Kudhibiti Ukimwi Zanzibar (ZACP) mwaka 2007 kiwango cha maambukizi miongoni mwa watumiaji wa Madawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga sindano (IDU) ni asilimia 16.0, kiwango cha maambukizi miongoni mwa wanawake wanaofanya biashara ya ukahaba (CSW) ni asilimia 10.8 na miongoni mwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao(MSM) ni asilimia 12.3 tofauti na kiwango jumla cha maambukizi kwa jamii ambacho kipo chini ya asilimia moja (asilimia 0.6).
Mapema bwana Nuhu Salanya, mwakilishi wa kanisa la Anglican katika jumuiya ya ZIADA aliwataka viongozi wa dini wasiogope kukubaliana na watu wanaofanya matendo maovu katika jamii kwa sababu hiyo ndio kazi yao.
“Kazi yetu kama viongozi wa dini ni kushughulikia matatizo ya kitabia miongoni mwa wafuasi wetu na kushawishi mabadiliko chanya kwa matendo hayo kupitia imani za kiroho” alisema Bw. Salanya .
Mapema wajumbe waliohudhuria mkutano kama huo katika ukumbi wa uwanja wa Gombani wetu wamepata moyo kuona kuwa harakati wanazoziendeleza kupitia misikiti, madrassa mihadhara na mikusanyiko ya kiajamii zimeanza kuzaa matunda ikiwa ni pamojana kudhibiti kasi ya maambukizi nakuifanya ibakishe chini ya asilimia moja (0.6) kwa zaidi yamiaka mitatu. mwisho

Friday, April 30, 2010

Utumiaji Endelevu wa ARV Unahitaji Kupewa Mkazo Zanzibar



Na Ali Haji Hamad, Pemba Press Club
Tunapozungumzia hadithi ya mafanikio katika mapambano dhidi ya Ukimwi katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la Saharahuwezi kuacha kuzungumzia nchi ya Uganda.

Ni nchi hii ambayo mwishoni mwa miaka ya themanini na katikati ya iaka ya tisiini ilikuwa na kiwango cha maambukizo kilichokuwa kinavuka asiimia ishirini.Lakini katika miaka hii wamefanikiwa kurejesha sio tu kiwango cha maambukizo hadi asilimia sita lakini pia wamefanikiwa kudhibiti kiwango hicho kwa miaka mitatu mfululizo.

Kuna mambo ambayo yamesaidia upande kuyafikia mafanikio hayo. Miongoni mwao ni kuwepo kwa Seraya madhubuti na zinazotekelezeka za kupambana na Ugonjwa huo, na kuwepo kwa taasisi imara zilijitolea kwa hali na mali kupambana na maambukizo ya virusi vya ukimwi na ukimwi na pia kutoa huduma kwa watu walioathiriwa kwa njia moja ama nyengine na ugonjwa huo.

Taasisi hizi zimetofautiana na nyengine kama usiku na mchana na taasisi zetu za hapa Tanzania ikiwemo Zanzibar ambazo nyingi lengola mwanzo huwa ni fedha na Mapambano ya Ukimwi huwa ni njia ya kuzifikia fedha hizo.

Tofauti na taasisi zetu nyingi zile za Uganda daima zimo kwenye harakati za kubuni na kutekeleza mikakati na mipango mipya itakayohakikisha mafanikio katika mapambano dhidi ya maambukizo mapya ya au utoaji bora wa huduma.

Miongoni mwa taasisi ambazo ziejijengea majina katika mapambano hayo nchini. Upendo na sasa kimataifa ni The Aids Support Organization (TASO).

The Aids Support Organization (TASO)
Jumuiya hii toka ilipoanziswa mwaka 1987 ilikuwa na lengo moja kubwa na imekuwa ikiisha kwa miaka zaidi ya ishirini kukamilisha lengo hilo. Lengo lenyewe ni kuchangia katika mchakato wa kukinga maambukizi ya virusi vinavyosababisha Ukimwi, kurejesha matumaini na kuboresha kiwango cha maisha cha watu , familia na jamii zilizoathiriwa na virusi vinavyosababisha Ukimwi.

Inakuwa ikifanya kila hali taasisi hii isiyo ya kiserikali kuhakikisha hili linafikiwa.

Mambo hayo ni pamoja na:-
Kutowa huduma za ushauri nasaha .
Kutoa huduma ya matibabu,huduma na kutowa msaada wa vitu.

Katika hayo yanayofanywa na Jumuiya za Uganda na hasa hiijumuiya ya TASO mimi nimevutika na huduma ya matibabu au dawa za kuongeza maisha kama tunavyopenda kuziita hapa kwetu.

Kilichonivutia hapa sio tu kwamba kazi za kutoa matibabu wa kuwarefusha maisha unatolewa na jumuiya hata zisizo za kiserikali bali pia ni jinsi huduma zenyewe zinavyotolewa. Nimeamua kuieleza hapa nikiamini labda wahusika wa tasisi zetu za kiserikali na zisizo za kiserikali wanaweza kuona mapungufa yao na kuchukua yale yaliyo mema na kuyatekeleza kwa ajili ya ndugu jamaa na marafiki zetu wanaoishi na virysi vya Ukimwi.

Katika utoaji wa matibabu ya kurefusha maisha (Anti -Refroviral Therapy) jumuiya hii imekwenda mbali zaidi ya kile tunachokifanya sisi hapa kwetu. Sisi tunachokifanya ni kutoa matibabu haya kwa wle watu wanaopaswa kupata na hapo wajibu wa wtoa huduma hizi ndio huwa umeisha. Kinachofanywa na jumuiya ya TASO kwanza ni kuhakikisha wale wote ambao wameandikishwa na jumuiya hiyo kama wateja wao wanapata huduma hizo na wanazitumia.
Pia sio tu kuzitumia lakini ni kuzitumia vile inavyopaswa na kila inapopaswa.

Community ART Support Agents ( CASA)
Katika kuhakikisha hili linafanikiwa TASO imeanzisha utaratibu maalum wa kuwatumia wateja wenyewe (watu wanaoishi na virusi vya ukimwi) kuhakikisha matumizi sahihi ya ART. Watu hawa wanaoitwa Community ART Support Arents hupatiwa mafunzo maalum ya kuyafaha matumizi ya ART. Nbaadae kuchaguwa wao wenyewe ni nani kati yao awe mwakilishi na msimamizi wao. CASA hawa kwa mujibu wa mmoja wao. Matilda Otim (Sio jina lake halisi).Wanapatiwa mbali na taalumavifaa vya ufuatiliaji kama vile baiskeli, rain suits gomboots na simu kwa ajili ya mawasiliano. hawa kazi ambayo wanaifanya ni kuhakikisha wanamtembelea kila mtu ambae anatumia ART katika eneo lao kumkumbusha kwanza kutumia dawa, pili kutumia dawa kwa usahihi na tatu katika wakati unaofaa.

Ndani ya zoezi hili CASA huyu huwakumbusha wateja hawa tarehe yao ya kuchukua dawa nyengine (drug re-fill). Kwa bahati njema dawa hizi pia husogezwa na wafanyakazi wa TASO katika eneo lililokaribu nao. Zoezi hili huwahakikishia wateja hao matumizi endelevu ya ART na hivyo kuboresha afya na kuwarejeshea matumaini ya kuishi na uwezo wa kufanya kazi za kujikimu. Kwa Mujibu wa Judith Okollo. Mfanyakazi wa kituo cha TASO Gulu pale inapotokezea kuwa mteja alietembelewa ni mgonjwa na anahitaji huduma ya haraka basi CASA hupiga simu ya Hotline katika Kit6uo cha TASO kilichokaribu. Hapo TASO hutuma gari yake maalum iliyowokwa kwa huduma ya Hotline kumfuta mgonjwa huyo na kumfikisha Hospitali. Ni uwajibikaji wa aina hii ndio unaoifanya jumuuiya kama TASO na Uganda kwa jumla kupata mafanikio ya kipekee katika mapammbano dhidi ya Ukimwi.

Yanayofaa kuigwa na Zanzibar
Nimeona hili ni jambo la kufaa hapa kwetu Zanzibar kwa sababu Zanzibar nayo ina miaka zaidi ya mitano tokea kuingia tokea imeingia kwenye huduma za Utoaji ARV bure. pamoja na taarifa za kuwepo kwa mwitikio mdogo wa Watu kutumia dawa hizi pia kuna tatizu la uendelevu wa matumizi hata kwa wale wachache ambao wamejitokeza kutumia.

wapo watu wanaoogopa kutumia ARV kwa kufuata uvumi tu kwamba zina madhara na zinzasababisha ugonjwa zaidi na kwa wengeine wanaogopa ule utumiaji wa dawa hizo kila siku. hata hivyo cha kusikitisha ni pale ambapo watu walioanza kutumia wanapoamua kukatisaha matumizi hayo. Wengine kwa kuona afya zimekuwa nzuri. Wengine kwa kuona hali zaohaziendi harakka kama walivyotarajia na Wachache kwa kushauriwa na waganga wa kienyeji kwamba wana dawa zenye uwezo wa kuponya badala ya kupunguza makali tu ya ugonjwa wenyewe.

wakati mtu anaweza kuwashushia lawama watumiaji weneyewe kwa upande mmoja, kwa upande mwengine tunapaswa kuzilaumu taasisi zetu zinazohusika utoaji na matumizi ya ART na kwakuwa hadi sasa kazi ya kununua na kusambaza bado inadhibitiwa na Wizara ya Afya hapa zanzibar basi labda tuilaumu wizara ya Afya kwa kushindwa kutumia drug adherence (matumizi endelevu ya dawa).

Kutoa dawa tu kwa watu wenye virusi vya ukimwi na baadae kuwaacha tu wenyewe watumie ni sawa na kujenga jengo zuri halafu ukaliachia watu watumie kwa wanavyojisikia bila usimamizi wa karibu. kwa vyovyote vile jengo hili haliwezi kubakia na uzuri wake huo bila kusimimia matumizi yake.

Watumiaji wa dawa za kurefusha maisha huwa wanahitaji ufuatiliaji wa karibu sio tu kwa sababu wanatatizo la kusahau lakini kwa sababu wanahitaji ushauri nasaha mara kwa mara kwa vile utumiaji wa dawa hizi ni wa maisha.

Jambo hili Jumuiya kama TASO waliliona mapema na ndio maana wameweka suala la ushauri nasaha kuwa ni sehemu ya program ya ART. Ili kuhakikisha kufani8kiwa kwa hili TASO huhakikisha kuwa wale wanaowatemebelea watumiaji CASA basi wenyewe wanaujuzi wa utoajai wa ushauri nasaha pia. Katika kuhakikisha hili limefikiwa taasisi kama TASO imekwenda mbali na kuanzisha huduma za kuwatemenbelea watumiaji wa ART majumbani (Home Visit). Hili sio tu kwamba inawafanya wajihisi nao wanajalia bali ni fursa tosha ya kuyaona mazingira yao halisi ya wananachi hawa tofauti na yale tunayoyaona wanapokuja Kliniki.

Kwa kuwatembelea katika maeneo wanamoishi pia tunapata nafasi ya kufahamu mahitaji ya ziada ya watu wanaoishi na virusi. Ni kutokana na huduma hizi ndipo hii miradi inayotekelezwa na baadhi ya taasisi iliweza kuibuliwa. Miradi kama vile ya kutoa huduma za vifaa vya shule kwa mayatima wa Ukimwi, Huduma za vyakula kwa watu wanoishi na virusi vya Ukimwi na hata zile za kuanzisha miradi midogo midogo imeibuiliwa uganda na kwengineko kwa uwajibikaji wa wazi wa aina .

Taasisi zetu zibadilike
Pamoja na mazoea yetu ya kutaka ufadhili katika takribana kila jambo tunalolifanya, jambo moja ni wazi juu ya hili kwamba tunahitaji kubadilisha kidogo tua mwelekeo wetu wa kuwahudumia watu wanaoishi na virusi vya ukimwi.

Kwa taasisi kama TASO hakuna muathirika bali kila mtu anaeishi na virusi na Ukimwi kwao huitwa mteja (client) Jambo hili huwapa moyo wa kuwahudumia kwa bidii zote kawani kama watu wasemavyo mteja ni mfalme.

Hata kama sisi kwa uwezo wetu wa kifedha hatuwezi kuwahudumia kama wafalme kama ndugu ,jamaa, marafiki, dada na ndugu zetu. Wizara ya Afya ya zanzibar na taasisi zinazotoa huduma za kinga, matibabu na huduma kwa watu wanoishi na virusi vya UKIMWI zizidishe nazo huduma za ushauri nasaha na kufikiria kuanzisha kwa mpango maalum wa watoaji na wafuatiliaji wa huduma za ART majumbani. Ni mikakati ya aina hii ndio iliyoifanya Uganda leo hii kuwa kielelezo cha mafaniko katika mapambano katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara. hata kama utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na TACAIDS umeionesha Zanzibar kuwa na maambukizi jumla ya chini ya asilimia moja bado tunawajibika kuwaka mikakati ya kuhakikisha kuwa asilimia hii haiongezeki na hao ambao tayari wameambukizwi basi wanapatiwa huduma za kufaa na kuishi kibinaadamu.

Mabadiliko ya Tabia nchi na Mwitikio wa Zanzibar katika Kukabiliana na Athari zake


Mabadiliko ya Tabia nchi na Mwitikio wa Zanzibar katika Kukabiliana na Athari zake

Na Ali Haji Hamad, PPC
Sasa ni dhahiri pengine kwa kila mtu kwamba mabadiliko ya tabia nchi (Climate change) ni miongoni mwa mambo yanayotishia ustawi wa maaendeleo ya mwanaaadamu na mustakbali wa maisha yake kuliko mambo yengine yote yanayohusiana na mazingira katika siku za hivi karibuni.
Hebu natuangalie mfulizo wa vimbunga vinavyotokea duniani katika siku za hivi karibuni kikiwemo kile kilechozikumba nchi za Europe na kugharimu maisha ya watu zaidi ya 50, tutizame mfululizo wa matetemeko hasa kwanchi ziliopo karibu na bahari kama vile Haiti tetemeko linakisiwa kuathiri maisha,malina makazi ya watu zaidiya200,000. Hayo ni mbali ya Ongezeko la kutisha la joto duniani. Wazanzibari wao walikuwa mashahidi wa ongezeko kubwa la joto pale umeme ulipokosekana kwa muda wa miezi takriban 3 katika visiwa vya Zanzibar.
Pengine kwa tabia za mwanaadamu za kuamini zaidi yale mambo anayoyaona kwa karibu anaweza kuyachukulia mambo tuliyotaja hapo juu kuwa ni matatizo ya mbali na yeye haya mhusu sana. Japo kudhani hivyo mara nyingi inaweza kuwa sawa ila si mara zote na hasa kwa hili tatizo la tabia nchi. Dunia hii ni moja kama ulivyo mwili na kikiumwa kidole cha mguu basi utatangaza maumivu kwa mwili nzima.
Mabadiliko ya tabia nchi na Mkulima wa Zanzibar
Pengine mtu aliyepo Zanzibar anaweza kujiuliza mimi kama Mzanzibari Mabadiliko ya Tabia nchi yamenigusa vipi’ jibu la hili litategemea wewe unafanya shughuli gani japo mwisho wa siku utakuwa umeguswa kwa njia moja au nyengine kwa shughuli yeyeote utayokuwa unafanya.
Tujaalie wewe ni Mkulima wa mpunga ulioko kijijini mbali huko pengine Mchangamdogo, ukitaka kujua ni kwa vipi mabadiliko ya hali ya hewa yamekugusa hebu fumba macho kidogo na uanze kukumbuka ni wakati wa mwaka ulikuwa unapata mvua za kusilia mpunga za kupalilia na kiangazi cha kuivisha mpunga uliokwisha fumua.
Hebu fikiri bonde ambalo ulikuwa unalitumia kwa shughuli zako za kilimo cha mpunga lilikuwa na maji au unyevu unyevu kiasi gani na kwa sasa hali ikoje, fikiri pia ulikuwa unapata mvua kiasi gani kwa mwaka na sasa hali ikoje. Sasa fumbua macho yako na uoene uhalisia bila shaka utagundua kuwa mambo yametofautiana na kuachana kama vile ardhi na mbingu.
Pengine wewe si mkulima wa mpunga ni mkulima wa muhugo, basi nawe jaribu kujikumbusha tu kidogo hali ilivyokuwa katika siku zako za awali za ukulima wa muhogo hebu kumbuka jinsi ambavyo ulikuwa na uhakika wa mazao mara baada ya kupanda kisiki chako na kukipalilia. Ulikuwa na uhakika iwapo umekipanda katika msimu wa mvua za vuli basi kingepata mvua za mchoo kidogo napengine za mwaka kidogo na baadae unang,oa muhogo wako sasa sina shaka kwamba wewe ni shahidi kwamba hali haiko tena hivyo. Kisiki cha muhogo ukikapanda leo kitategemea zaidi mvua hiyo uliyoipandia na mara nyengine hiyo huwa ndio ya mwisho. Hakuna tena uhakika wa mvua hata katika ile miezi iliyojulikana kwamba ndio msimu wake.
Mabadiliko ya tabia nchi na Mfugaji wa Zanzibar
Hata wafugaji pia nao wanaweza kushuhudia kwa upande wao athari hizo za mabadiliko ya tabia nchi pengine bila hata kusubiri tafiti za kitaalamu. Wao na waangalie tu pale ambapo walikuwa wakipeleka mifugo yao kunywa maji katika vijito vilivyokuwa vimeenea katika maeneo ya kuchungia mifugo yao jee bado mna maji humo. Hebu na waangalie pia aina na wingi wa majani waliokuwa wakiupata kwa ajili ya mifugo yao bado yapo. Ninahakika jibu litakuwa ni hapana. Hizo ndizo athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Hapa kwetu Zanzibar halijatokea lakini kwa wafuatiliaji wa vyombo vya habari ni mashahidi wa migogoro isiyo kwisha baina ya wakulima na wafugaji migogoro ambayo mara nyengine huleta vifo. Wafugaji wanatangatanga na mifugo yao wakitafuta chakulisha huku wakulima wakilinda mazao yao. Kwa ukosefu wa malisho wafugaji hudiriki hata kuhama kabisa katika mikoa yao na kuhamia mikoa jirani au mara nyengine kuvamia maeneo ya hifadhi.Hilo halikuwepo zamani.
Mabadilikoya tabia nchi na wewe
Kama wewe si mkulima wala mfugaji lakini ni mkaazi tu wa maeneo ya ukanda wa pwani ya Tanzania vikiwemo visiwa hivi vya Zanzibar au pengine ni mtembezi tu wa maeneo hayo nawe unanafasi ya kuwa shuhuda wa athari za mabadiliko ya tabia nchi. Kama ni mkaazi wa Tanzania bara hebu waulize wavuvi wa Kikojani wakuoneshe pale ambapo walizoea kujenga mabanda kwa shughuli zao za dago katika eneo la Kunduchi. Bila shaka huwezi kuamini kwa sababu eneo lote hilo sasa nia sehemu ya bahari.
Lakini ikiwa hupendi kuamini kauli za wavuvi jaribu uwaulize wamiliki wa hoteli ya kundichi wakuoneshe pale maji ya bahari ambapo miaka kama kumi iliyopita yalikuwa yanaishia na jinsi sasa yanavyowapigia hodi pamoja na jitihada zao za kuweka mawe ya kuzuia kasi ya mawimbi katika maeneo mbali mbali.
Kama upo Zanzibar nenda tu katika fukwe iliyokaribu nawe ambayo ulikuwa na tabia ya kuitembelea hapo zamani uone hali ikoje. Wananchi wa Vijij vya tumbe, Kukuu, na msuka ni mashahidi wa zuri wa athari hizi za kupanda juu kwa maji ya bahari ambayo ni moja ya athari za mabadiliko ya tabia nchi kwakuwa hata baadhi ya maeneo yao ya kilimo yameanza kuathiriwa na maji ya chumvi.
Athari hizi ni mbali ya zile za tishio la kumezwa kwa baadhi ya visiwa vidogo vidogo viliomo ndani ya bahari yeteu kama ambavyo aliwahi kutahadharisha waziri kiongozi wa Zanzibar Mhe. Shamsi Vuai Nahodha wakati akifunga kikao cha Baraza la Wawakilishi mwishoni mwa mwaka uliopita.
Mifano hii na mengine mingi ikiwemo ile ya ongezeko la mardhi ya joto kwa binaadamu kama vile malaria, upele wa joto na fungus na maradhi ya wanyama ambayo tukiyaorodhesha hapa hapa itachosha. Mifano hii naitoshe kuonesha angalau zile athari za moja kwa moja ambazo kama binaadamu, kama Watanzania na kama Wazanzibari zinatukabili kutokana na mbadiliko ya tabia nchi.
Jee tumechukua hatua kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi?
Athari ndio zipo na uwepo wake ni dhahiri suala la kujiuliza ni jee tunafanya nini kukabliana na athari hizi ziliopo au kukinga athari zaidi zinazo weza kujitokeza. Tunaweza kujiuliza suali hili kama wananchi mmoja mmoja wakaazi wa Zanzibar, tunaweza kujiliuliza suala hili kama sehemu ya taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali zenye wajibu wa kuleta ustawi wa wananchi na tunaweza kuliuliza suala hili kwa serikali kuu.
Mimi sina jibu la moja kwa moja ila nilidhani suala hili ni muhimu kulileta hapa ili liwe changamoto kwetu sote. Kwa Yule ambaye amechukua hatua achukue zaidi na Yule ambaye hajaanza basi aanze sasa japo ukweili ni kwamba tumechelewa kidogo.
Wananchi
Kwa wananchi mmoja mmoja au labda niseme jamii yenyewe imefanya jitihada kwa kiasi chake cha kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa yale maeneo husika. Kinachokosekana kwao ni ule msukumo wa kuzifanya jitihada zao zilite mafanikio makubwa.
Kwa mujibu wa maelekezo na tathmini za kitaalamu mkulima aliefahamu kwamba sasa akipanda mbegu ya muda mrefu ya muhogo hawezi kupata mafanikio kwa hiyo akachukua hatua za kutafuta mbinu mbadala na kuanza kupanda muhogo wa miezi sita badala ya mwaka huyo anahesabiwa amechukua hatua ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa kuwa hili linafanyika ndio mana nasema wao wameanza kuchukua hatua.
Kwa mfano kwa wale wanaotokea upande wa mkoa wa Kaskazini pemba nadhani na hata Kusini pia wao ni mashahidi wa jinsi wakulima wa muhogo wa huko walivyopagawa na kupanda mbegu inayojulikana kwa jina la sepideh badala ya mbegu ya kibiriti. Sifa kubwa ya mbegu hii ni kwamba muhogo wake unamea na kulika haraka. Wakulima wenyewe wanasema kuanzia miezi mitano hadi sita unaanza kula na miezi tisa ndio muda wake wa juu zaidi wa kubakia.
Japo nilipomuuliza Ali Bakar Hassan (27) mkaazi wa kijiji cha Kairo Mchangamdogo kwa nini wameamua kuachana na mbegu za muda mrefu jibu lake halikutaja moja kwa moja mabadiliko ya tabia nchi lakini mantiki yake ilielekeza huko. “ Hizi ndizo mbegu zinazotufaa siku hizi, (mbegu za muda mfupi) ukipanda visiki vikipata mvua moja, tu miezi sita utang’oa muhugo ule na wanao lakini kibiriti mwaka mzima wasubiri, ukikosa mvua hamna kitu” alisema Ali Bakar
Kwa hiyo hilo ni eneo moja ambalo jitihada za kijamii za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi zinaonekana , eneo jengine ni hili la upandaji miti. Katika siku za hivi karibuni limekuwa jambo la kawaida kuwasikia wananchi wa shehia fulani za ukanda wa pwani wa visiwa wamekaa pamoja na kufanaya shughuli za upandaji wa mikoko. Hili ni jambo muhimu pia kwani mikoko infanyakazi nyingi kwa pamoja katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi. “Inafanya kazi kama ngao ya kukabiliana na mawimbi makubwa yanayopelekea mmong’onyoko wa fukwe au kupanda juu kwa maji ya bahari Inasaidia pia upatikanaji wa kuni na kupunguza shindikizo kwa ukataji wa miti mengine na uchomaji mkaa” aliniambia Moh’d Said wa jumuiya ya kuhifadhi mazingira ya pwani ya Kojani KOYMOCC kuthibitisha kuwa wanajua wakifanyacho pale wanapoamua kupanda mikoko. Wataalamu wao wanasema inasaidia kutoa hewa safi na kusaidia kufyonza gesi mkaa (Carbondioxide) ambayo ni chanzo kikuu cha mabadiliko ya tabia nchi.
Jitihada hizi za wananchi za kupanda mikoko zinaonekana katika vijiji kama vile Shumba mjini, Micheweni, Kangani, Fundo, Tumbe na vingi nyenginezo.
Jitihada hizi ni mbali ya zile zilizozoeleka za kwa mfano kupiga matuta makubwa ya kuzuia maji ya chumvi yasiingie kwenye mashamba yao ya kilimo kama inavyoonekana katika maeneo ya bandari ya Tumbe na Kangani Pemba.
Taasisi
Wakati sina vyema kubeza jitihada za kitaasisi za kukabiliana na mabadilio ya tabia nchi kwa mtazamo wango nadhani eneo hili bado halija fanya kazi ya kutosha yakukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa mfano taasisi ambazo zinahusika na kilimo ama usimamizi wa kilimo nilizitarajia ziende mbali zaidi. Ziende mbali kwasababu zinafahamu kwamba hali ya mvua sasa si ya kuaminika.
Nilitarajia kwa kulifahamu hilo taasisi zielekeze nguvu zake katika kilimo cha umwagiliaji ili uzalishaji wa mazao kama vile mpunga na mbuga mboga uendelee bila kuathiriwa na mvua ambazo sasa zimekuwa si za kuaminika tena. Hata hivyo badala ya kupanuka zaidi kwa maeneo ya umwagiliaji kinachoshuhudiwa sasa ni kupungua hata kwa yale maeneo ya umwagiliaji yaliyozoeleka kumwagiliwa. Kwa mfano, binafsi nilizoea kuliona eneo la Mtaka kaa Mtambile likilimwa kilimo cha umwagiliaji na kutoa matunda mazuri lakini sasa linalimwa kwa kutegemea mvua. Hali ni hivyo pia katika eneola Darajani Tumbe na eneo la Kicha Kinowe. Nataja maeneo hayo machache kwa sababu yanaonekana mara kwa mara.
Eneo jengine ambalo nadhani taasisi hizi zingeweza kuwasaidia wananchi kufanya vizuri katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ni kuazinsha utaratibu wa kuvuna maji yamvua. Hadithi ya umuhimimu wa kuvuna maji ya mvua imekuwa ya sikunyingi lakini isiyo na mafanikio. Nadhani wakati huu ni muhimu zaidi kuliko wakati mwengine wowote kuhakikisha jambo hili linatekelezwa na kuleta mafanikio. Taasisi hizi zikiwemo zile za kibinafsi zinaweza pia kusaidia kwa kuanzisha kampeni maalum ya kuwahamasisha wananchi kuhifadhi vyanzo vya maji walivyo navyo na mabwawa ya kimaumbile ya kuhifadhi maji kama vile maziwa badala yakuyafukia.
Kwa mfano kwa wakaazi wa Pemba wanafahamu kwamba shehia za Ole na Kangagani zilikuwa zinasifika sana kwakuwa na idadi kubwa ya mabwawa ya kimaumbile yakuhifadhimajiya mvua. Wakati mvua kubwa za masika zinaponyesha maji yanayotoka mitaani na mabonde yalikuwa yanaishia kwenye mabwawa hayo na kuhifadhika kwamuda mrefu. Wananchi wao waliyatumia mabwawa haya kwa shughuli zakijamii za kawaida kama vile kuogea, kufulia nguo, kuvua samaki, na kumwagilia mboga mboga. Hata hivyo mabwawa haya ama maziwa kama wanavyoyaita watu wa huko sasa yameanza kupotea moja baada ya moja.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa jumuiya ya Kiraia ya kuelimisha matumizi endelevu ya ardhi na Mazingira (PALESO) Mbarouk Hamad Yussuf jambo hilo husababishwa na ukulima mbaya unaofanywa pembeni ya maziwa hayo na hakuna mkakati wowote wa kuwakumbusha wananchi wa maeneo haya umuhimu wa kuyataunza mabwawa haya katika kipindi hichi ambacho dunia inakabiliwa na hali ngumu yamabadilikoya Tabia nchi.
Serikali
Serikali kama serikali pengine kwa upande wake imetekeleza sehemu kubwa ya jukumu lake. Kwa mfano imekuwaikifanya jitihada za kuwasomesha wataalamu ili waweze kusaidia ushauri wa kukabiliana na hali hii.Imekuwa ikitandika sera imara za kukabiliana na uharibifu wa mazingira, na imekuwa ikiwaasa wananchi juu ya hali hii. Lakini nayo nadhani bado ina nafasi kubwa ya kupunguza athari hizi zamabadiliko ya tabia nchi.
Kwamfano kuna mikataba ya kimataifa ya kukabiliana na hali hii ambayo serikaliinaweza kuingia ili nayo ifaidike na jitihada za kimataifa za kukabiliana na Climate change. Kuna miradi ya kupunguza gesi joto (Clean Development Mechanism) ambayo kila nchi ikiwemo Tanzania imepewa fursa ya kuanzisha na kutumia faida zake. Pamoja na kwamba tayari Tanzania imeanzisha miradi 12 ya aina hiyo ikiwemo ile ya Mradi wa kuzalisha umeme kupitia dampo la Mtoni na Mradi wa kuzalisha umeme kupitia mabaki ya Mkonge wa Hale Tanga lakini kwamujibu wa habari zilizopatikana toka kwa Mkurugenzi wa taasisi ya Teknolojia, Nishati na Sayansi ya Mazingira (CEEST) yenye makao yake makuu Dar es Salaam Hubert Meena na kuthibitishwa na Idara ya Mazingira iliyochini ya Afisi ya Makamo wa Rais wa Tanzania inayoratibu miradi ya aina hiyo, Zanzibar bado haijatumia fursa hiyo. Hilo ni eneo ambalo serikali kuu inaweza kuingiza mkono wake kwa angalau kuwatafuta wawekezaji wa miradi ya aina hiyo.
Eneo jengine ambalo serikali inaweza kutoa msukumo ni kuviunga mkono kwa hali na mali vikundiambavyo vinafanya jitihada ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya vikiwemo vilevikundi vinavyojishughulisha na upanadajimitihasa ile ya mikoko. Vikundi hivi vinafanya kazi hii bilamsaada wowote na vingivyao vinaishia kukata tamaa na kuacha kufanya kazi hiyo. Labda kama kwa suala la uwezo serikali inashindwa kutekeleza hilopekee inaweza hata kuilekeza baadhi ya miradi inayojishughulisha na mazingira kama vile mradi wa Matumizi Endelevu ya Ardhi na Mazingira (SMOLE) ambao hivi karibuni ulitajwa kuanza tena awamu nyengine hap Zanzibar katika kuviunga mkono vikundi vinavyojishughulisha na uhifadhi wa mazingira hususana vinavyolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia.
Kumalizika kwa mkutano wa Copenhagen – Denmark wa mwezi Decemeber 2009 bila maazimia ya maana ya miongoni mwa mataifa makubwa juu ya kukabiliana na tatizo la tabia nchi iwe funzo kwetu kwamba ni wakati sasa wa kujaribu kufurukuta wenyewe kukabiliana na tatizo hili. Tusisubiri wengine waje kuomba kutusaidia, “cha kugaiwa huja jioni,watu ndivyo wasemavyo”







Wanawake Micheweni Wageukia Kilimo cha Mbogamboga

WANAWAKE MICHEWENI WAGEUKIA KILIMO CHA MBOGA MBOGA

Na Ali Haji Hamad, Pemba Press Club

Baada ya kuvunjika moyo na kazi ngumu ya kilimo cha mwani na mapato madogo yanayopatikana katika kazi hiyo,wanawake katika wilaya ya Micheweni -Pemba sasa wameanza kugeukia kilimo cha mboga mboga kama njia ya kujiongezea kipato na kupambana na umaskini.

Wanawake hao kutoka shehia za Shumba mjini, Micheweni, Mjini wingwi, Njuguni na Mjananza wanajishughulisha na kilimo cha mchicha tungule, pipili mboga, mabilingani na vitunguu kama njia mbadala ya kujipatia kipato.

Katika shehia ya Shumba mjini ambako kwa miaka mingi iliyopita wananchi wa huko walikuwa wakidhani kwamba kilimo cha mboga mboga hakiwezi kustawi, sasa kuna zaidi ya vikundi vitano vya mboga mboga kwa mujibu kwa mujibu wa afisa wa mradi wa kuwawezesha wanawake Zanzibar WEZA, Jitihada Abdalla.

Mwenyekiti wa kikundi cha Mshikamano, mojawapo ya vikundi vya Shumba mjini bi Assaa Shapandu Makame amesema kuwa kikundi chao chenye wanachama 12 wote wanawake kimeanza kuona matunda ya kilimo hicho muda mfupi tokea kuanza na shughuli hiyo.

Amesema awali kikundi chao kilianza kama kikundi cha kuweka na kukopa chini ya mradi wa kuwawezesha wanawake Zanzibar WEZA hadi pale maafisa wa mradi huo walipowashawishi kujaribu kilimo cha mboga mboga ili kupata michango ya kuweka hisa badala ya kutegemea mwani pekee.

Amesema sasa wameanza kilimo cha mboga na wameanza kuvuna na kuweka kwenye kisanduku chao kiasi cha shilingi 20,000/=

Fatuma Kombo Ali, mwanachama wa kikundi hicho amesema japo kiwango cha fedha kinaonekana kidogo lakini faida ianyopatikana katika kilimo hicho ni kubwa kwa vile klilimo cha mboga mboga hakitumii muda mwingi na mwanamke anaweza kukiendesha bial kuathiri shughuli za utunzaji familia.

“Ukilima mwani siku nzima unakuwa hupo nyumbani, hujui wanao walalo wala wanywalo, na ukirudi hunachochote zaidi ya machoka. Lakini mboga walima muda mdogo na ukiondoka una kichacha kimoja cha kitoweo” alisema Fatuma

Katika kikundi cha Subira ni njema cha hapo hapo shumba bi Juma Makame amesema kikundi chao cha wanawake 13 ambacho nacho kinajishughulisha na kilimo cha mchicha na tungule wamefanikiwa kukusanya shilingi 70,000 katika jaribio lao la kwanza la mauzo.
“pesa tupatazo japoi si nyingi lakini na kazi tufanyayo nayo si kubwa kama ya mwani. Ukilima mboga mboga angalau wapata kufanya kazi nyengine za nyumbani”alisema

Bikombo Rashid Massoud mkazi wa Shumba mjini yeye ameamua kuendesha kilimo cha mboga mboga pekeyake bada ya kujifunza kutoka katika kikundi. Amesema anafanya hivyo ili kupata pesa pesa za kuweka hisa katika kikundi cha kuweka na kukopa cha mradi wao wa WEZA.

Amesema tokea kuingia katika kilimo hicho amekuwa na uhakika wa kujipatia shilingi 500 za kuweka katika kisanduku cha kikundi chao na ziada ya kutumia nyumbani.

Kuhusu soko la mboga mboga Bikwao Massoud Ali, mwanachama wa kikundi cha Wezarohoyo cha Mjiniwingwi amesema soko la mboga mboga katika Wilaya ya Micheweni lipo na nila uhakika kuliko soko la mwani. Amewaomba watu wa mradi wa WEZA na miradi mengine ya kuwaendeleza akina mama kuwasaidia kwa karibu akina mama wanaojishughulisha na kilimocha mboga mboga kwa kuwajengea miundo mbinu ya umwagiliaji ile waweze kuendesha kilimo hichi kwa mwaka mzima.

Mapema Jitihada Abdalla alifahamisha kuwa mradi wa WEZA ambao unaendeshwa
kwa pamoja na Shirika la CARE Austria na Chama cha Waandishi wa habari Wanawake TAMWA amesema katika mwaka huu mradi huu umeweka mkazo maalum katika kuwawezesha wanawake kijamii na kiuchumi huku ukiwahimiza kuendesha miradi yenye kuleta mafanikio ya haraka kwa ili kuwaongezea kipato chao na kuimarisha mchango wa sekta hiyo mkatika uchumi.

Wednesday, April 28, 2010

Refusheni Muda wa Matumizi ya ARVs kwa Wanyonyeshaji

Na Ali Haji Hamad Cape Town,2009
Hatari ya maambukizo ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto inapunguwa kwa kiwango kikubwa iwapo mama mnyonyeshaji anaeishi na virusi vya ukimwi atarefushiwa muda wa matumizi ya dawa za kurefusha maisha (ARVs.)

Hayo ni kwa mujibu wa utafiti mpya wa Kukinga maambukizi mapya ya virusi viavyosababsha ukimwi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto uliongozwa na shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na kuendeshwa na Shirika la Utafiti wa Ukimwi la Ufaransa (ANRS) na Kituo cha Marekani cha Kinga na Udhibiti wa Magonjwa (CDC).

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo uliopewa jina la kiswahili la "Kesho bora" katika Mkutano wa Kimataifa wa Ukimwi unaofanyika Cape Town Mratibu wa kinga katika idara ya ukimwi ya Shirika la Afya Ulimwenguni Drk Yin - Ro - Lu amesema utafiti huo umetowa matumaini mapya katika kuzuia maambukizi mapya na vifo kwa watoto katika nchi na maeneo amabayo mama wengi wanaoishi na virusi vya ukimwi bado wanalazimika kunyonyesha watoto wao.

Amesema utafiti huu unaongeza nguvu kwa ule utaratibu wa awali uliokuwa unaruhusu kuwapa akinamama waja wazito wanaoishi na virusi vya ukimwi dawa za ARVs katika siku za mwisho mwisho tu za ujauzito wao na siku za mwanzo baada ya kujifungua.

Dk. Yin Amesema kwa utafiti huu mpya sasa akinamama waanaoishi na virusi vya ukimwi wataweza kupatiwa dawa za ARVs mapema zaidi katika ujauzito wao na kurefushiwa matumizi mpaka miezi sita baada ya kujifungua kama njia ya kukinga maambukizi kutoka kwa mama hao kwenda kwa watoto wao.

Aidha amesema utafiti huo ambao uliendeshwa kati ya June 2005 na August 2008 katika maeneo matano tofauti ya bara la Afrika na kuwashirikisha akina mama 1,140 wajawazito wanaoishi na virusi vya ukiwi, umegundua kuwa matumizi ya dawa hizo yanakuwa na matokeo bora zaidi ikiwa akina mama wajawazito wataanza kuzitumia wakiwa bado wana kiwango cha juu cha chembe chembe za kinga (CD4) za kati ya 200 hadi 500 (200-500cells/mm3).

Akielezea umuhimu wa ugunduzi huo kwa mataifa yanayoendelea alisema kwanza utasaidia sana kupunguza unyanyapaa unaowapata akinamama wanaoacha kunyonyesha watoto wao kwa khofu ya kuwaambukiza na pia kuondoa tatizo la sasa la watoto wengi kupata utapia mlo baada ya kuzuiwa kunyoyeshwa kutokana na familia zao kukosa uwezo wa kuwapatia mlo kamili au kupata utaratibu unaoubalika kimataifa wa kutoa mlo huo.

Kwa mujibu wa maelekezo ya sasa ya Shirika la Afya Ulimwenguni, inapendekezwa mama wanaoishi na virusi vya ukimwi wawanyonyeshe watoto kwa miezi yote sita ya mwanzo na iwe ni unyonyeshaji pekee bila mtoto kulishwa kitu chengine chochote isipokuwa katika mazingira mabayo utaratibu unaokubalika wa kulisha mtoto unapatikana,unawezekana, ni salama na utakuwa endelevu.

Hata hivyo kufuatia utafiti huu mpya Shirika la Afya Ulimwenguni linayapitia upya mapendekezo yake hayo ya mwaka 2006 na linatarajiwa kutowa maelekezo mapya mwishoni mwa mwaka huu 2009.

Chanjo Mpya ya Kifuakikuu Yaja

CHANJO MPYA YA KIFUA KIKUU (TB) YAJA
Na Ali Haji Hamad, Cape Town,2009
Shirika la kimataifa linalojishughulisha na utafutaji wa Chanjo dhidi ya Ugonjwa Kifua kikuu (TB) la AERAS Global TB Vaccine Foundation limesema limekuwa likipata mafanikio makubwaa katika jitihada zake za kutafuta chanjo mpya dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Raisi wa Taasisi hiyo Dr. Jerald Sadoff ameliambia jopo la waandishi habari 56 kutoka mataifa 40duniani wanaohudhuria mafunzoya Kimataifa ya ukimwi hapa Cape Towm kuwa tayari chanjo hiyo ambayo inasimamiwa pia na Chuo kikuu cha Oxford cha Uingereza na Tasisi ya Chanjo ya Kifua Kikuu ya Hapa Afrika kusini (South African Tuberculosis Vaccine Initiative) imokatika hatua ya pili ya majareibio ya ubora wake katika maeneo yaliyo athiriwa zaidi na ugonjwa huo.

Akitoa ufafanuzi kuhusu chanjo hiyo inayojuilikana kwa jina la MVA85A/AERAS-485 Dr. Sadoff alisema inakusudia kuongeza nguvu ya chanjo inayotumika sasa ya Bacille Calmette- Guerin (BCG) ambayo inaonekana kutokufanya kazi vyema hasa katika kukinga Kifua kikuu cha kwenye mapafu na kwa watoto walioambukizwa virusi vya ukimwi.

Alisema chanjo ya sasa ya BCG ambayo ilivumbuliwa miaka 90 iliyopita pamoja na kutumika kwa kiasi kikubwa kuwakinga watoto dhidi ya maambukizi ya kifua kikuu kote duniani haijasaidia sna kupunguza idadi ya watu wanaouguwa kifua kikuu na akasema kwamba dunia kwa sasa inawatu wengi zaidi wanaouguwa kifua kikuu kuliko wakati mwengine wowote.Mwaka 2007 pekee watu 9,270,000 waliuguwa kifua kikuu kote duniani na watu 456,000walipoteza maisha jamboambalo linaufanya ugonjwa huokushika nafasi ya pilikwa kuuwa watu wengi baada ya ukimwi.

Dr. Sadoff amesema Chanjo mpya ambayo inatarajiwa kuwa tayari kutumika baada ya miaka mitano tayari imetolewa kwa watoto 2784 wa Afrika kusini kuangalia ubora wake katika kukinga na hatua hiyoitafuatiwa na hatua ya tatu ya majaribioya jumla yatayowajumuisha watu wengi zaidi na wa rika zote.
Akizungumziamahusiano ya kifua kikuu na Ukimwimwanasayansi huyo alisema kuongezeka kwa maambukizi ya Ukimwi duniani kumeifanya kazi ya kupambana na kifua kikuu kuwa ngumu zaidikwa vile idadi ya wagonjwa imeongezeka pia na vijidudu vya kifua kikuu inakuwa tabu kugundulika katika hatua z awali kwa watu walioambukizwa virusi vya ukimwi.

Takwimu zinaonesha kuwa katika kila watanzania 100,000 (laki moja) kuna watu kati ya 100 - 299 wanaougua Kifua kikuu.
Mbali na Ukimwi mtaalamu huyo ameyataja mambo mengine yanayochochea kukuwa kwa tatizo la kifua kikuu kuwa ni Uvutaji Sigara, Ugonjwa wa kisukari,Msongamano wa watu na Umasikini wa kupindukia ambaohuwafanya watu kushindwa kupata mlokamili.Mapema Mwanasayansi mwengine ambae ni mshauri mkuu wa Jumuiya ya kimataifa ya Kupambana na Ukimwi na Kifua kikuu (IUTA) Anthony Harries alitowawitokwa waandishiwa habarikusaidia kulifanya tatizola kifuakikuu kuwa ajenda kam ilivo ukimwi na mabadiliko ya tabia nchi kutokaqna na athari yake iliyonayo kwa maisha ya watu.



.


.

shamba la mikoko


ZANZIBAR YAACHWA NYUMA KATIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Na Ali Haji Hamad, Pemba Press Club

Ikiwa ni zaidi ya miaka 12 sasa tokea mataifa mbali mbali duniani yalipofikia makubaliano kupitia mkataba wa Kyoto ya kupunguza utojai wa gesi joto (Greenhouse gases) na kutoa fursa kwa mataifa yanayoendelea kuanzisha na kufaidika na miradi ya kupunguza gesi joto (Clean Development Mechanism) na athari za tabia nchi, hakuna mradi wowote ulioanzishwa wala kuombwa kutokea Zanzibar, imebainika.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka taasisi ya Teknolojia, Nishati na Sayansi ya Mazingira (CEEST) yenye makao yake makuu Dar es Salaam na kuthibitishwa na Idara ya Mazingira iliyochini ya Afisi ya makamo wa Rais wa Tanzania inayoratibu miradi ya aina hiyo, katika kipindi chote hicho Tanzania kwa jumla ina miradi 12 ambayo imo katika hatua mbali mbali za utekelezaji na maombi na kwamba hakuna mradi wowote unaotokea Zanzibar ama kupangwa kutekelezwa huko.

Mkurugenzi wa CEEST Hubert Meena aliwatajia waandishi wa habari za Mazingira waliokuwa wakihudhuria mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzanaia (JET) kwa mashirikianao na Thamson Foundation Jijini Dar es Salaam hivi karibuni Miradi ya Tanzania kuwa ni pamaoja na Mradi wa kukusanya gesi ya methane na kuzalisha umeme kutoka katika jaa la Mtoni kwa Azizi Ali Dar es salaam ambao umeanza kufanya kazi na Mraadi wa kuzalisha Umeme kutokona na takataka za mkonge wa Kijiji cha Hale -Tanga ambao ujenzi wake umekamilika na unasubiri kuthibitishwa.

Mkurugenzi huyo aliitaja miradi mengine kuwa ni mradi wa umeme wa Upepo wa Singida, Mradi wa Umeme wa kinyesi katika jela za Tanga, Arusha na Moshi, mradi wa gesi asilia wa Moshi, Miradi ya Upandaji misitu ya Mwanga na Same, Umeme wa biomass_ Tanga na Miradi ya nishati mbadala ya Mtwara na Lindi ambayo yote bado imo katika hatua za maombi.

Akithibitisha hali ya Zanzibar kutokuchangamkia miradi ya Upunguzaji wa gesi joto, Mtaalamu wa Mazingira kutoka Idara ya mazingira iliyochini ya Afisi ya makamo wa Rais ambayo pia inajukumu la kuratibu miradi yaaina hiyo, Bw. Fredy Manyika alisema katika suala la kukabiliana na ongezeko la gesi joto na athari za tabia nchi na kutekeleza miradi inyohusiana nayo Tanzania inafanya kazi kama nchi moja (Jamhuri ya Muungano) kwa vile ndiyo iliyoridhia mkataba wa Kyoto hapo 2002.

Hata hivyo alisema katika suala la maamuzi ya mradi upi wa kupunguza gesi joto utekelezwe wapi jambo hilo halihusiani na nchi moja kwa moja kwa vile miradi hiyo imeachwa kama fursa ya kiuchumi na kibiashara kwa kila nchi na utekelezaji wake utategemea jinsi wananchi, taasisi, wafanyabiashara na wawekezaji watakavyoichangamkia fursa hiyo kwa vigenzo vyao mbali mbali.

Alisema katika hali hiyo ni juu ya taasisi, wananchi, na wawekezaji wa Zanzibar ama pekeyao au kwa kushirikiana na taasisi nyengine za kimataifa kuomba na kutekeleza miradi mingi kadri wawezavyo wakizingatia faida za kibiashara, ajira, teknolojia na mazingira zitazopatikana.

Kwa mujibu wa taasisi ya Teknolojia, Nishati, na Sayansi ya Mazingira kwa kuacha kuchangamkia fursa ya utekelezaji miradi ya kupunguza gesi joto, nchi, mikoa, wilaya na maeneo hupoteza fursa kadhaa zikiwemo zile za kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi, kuongeza nafasi za ajira, upatikanaji wa teknolojia mpya na ukuaji wa uchumi kupitia biashara ya uuzaji wa Ankara za gesi mkaa (CO2) na methane iliyodhibitiwa .

Kwa mijibu wa taasisi ya CEEST kuna biashara ya zaidi ya dola za kimarekani 30 billioni kila mwaka katika nchi za jumuiya ya Ulaya kupitia miradi ya kupunguza gesi joto na athari za tabia nchi. Hubert Meena , Mkurugenzi wa kituo hicho alisema kwa sasa soko hilo linazinufaisha zaidi nchi za India , China , Brazil na Afrika ya Kusini.

Meena amliyataja baadhi ya m,aeneo ambayo taasisi ,wafanyabiashara , na wawekezaji wanaweza kuyatumia kuanzisha miradi ya kupunguza utoaji wa gesi joto na athari za tabia nchi kuwa ni pamoja na sekta ya Nishati amabayo inatoa fursa ya miradi ya kuzalisha umeme, kukuza teknolojia na kupunguza matumizi ya mafuta; Sekta ya viwanda inayotoa fursa ya miradi ya kupunguza gesi mkaa; Sekta ya Usafirishaji inayotoa fursa ya miradi ya kupunguza wingi wa vyombo vya uasafirishaji na kuongeza ufanisi wa usafirishaji; na Sekta ya Utupaji taka ambayo inatoa fursa miradi ya udhibiti na matumizi ya taka ngumu na maji taka.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kuna miradi 828 ya kupunguza gesi joto na athari za tabia nchi inayofanya kazi kote duniani na mengine 2,600 ambayo maombi yake yanashughulikiwa na kamati tendaji ya miradi ya aina hiyo. Kati ya miradi yote ambayo tayari imeanza kufanya kazi Afrika ina miradi 30 na zaidi ya nusu ya miradi hiyo iko Afrika kusini.

MWISHO
N.B Maneno mengine ni ya kisayansi nimekosa Kiswahili chake.
Hayo machache niliyoyapata tafsiri yake imetoka baraza la Kiswahili Tanzania .
Mabadiliko ya tabia nchi (Climate Change)
Gesi mkaa (Carbon dioxide)
Gesi Joto (Greenhouse gases)
Mobile: +255777458523