SciDev.Net

Pages

Thursday, July 22, 2010



RAS MKUMBUU PEMBA

RAS MKUMBUU YAPATA MRADI WA HIFADHI YA MAZINGIRA YA BAHARI

Na Ali Haji Hamad, Pemba Press Club
Eneo la bahari ya Ras Mkumbuu Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini- Pemba. Limechaguliwa kuwa mojawapo ya maeneo mawili ya Tanzania yatayoanzishwa mradi wa mfano (demonstration project) wa Uhifadhi wa Mazingira ya bahari na uendelezaji wa jamii iliyozunguka kupitia mradi mkubwa wa uhifadhi wa mazingira ya Bahari unaojulikana kwa jina Agulhas and Somali Current Large Marine Ecosystem Project (ASCLME)

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika tovuti ya Mradi huo, (www.dlist-asclme.org) utaofadhiliwa na Global Environmeantal Facility (GEF) na kutekelezwa na shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) mbali na eneo la Ras Mkumbuu – kisiwani Pemba eneo jengine la Tanzania ambalo limo kweneye mradi huo ni eneo la Kilwa Tanzania Bara.

Pamojana Tanzania Mradi wa ASCLME utaendeshwa pia katika nchi nyengine nane zikiwemo Afrika Kusini, Somalia, Kenya, Msumbiji, Madagasca, Mauritaus, Comoro na Seychelles kwamuda wa miaka mitano kwa gharamaza zaidi ya shilingi za Tanzania Bilioni 17 (US$ 12.2milioni)

Kwa mujibu wa tovuti ya mradi wa ASCLME eneo la Ras Mkumbuu ambalo lipokaribu kabisa na eneola hifadhi ya kisiwa cha Misali –Pemba limechaguliwa kutokana na kuwa kwake katika nafasi nzuri ya ki-jeografia na kuwa na utajiri wa matumbawe, aina mbalimbali za samaki na rasilimali ya viumbe vidogovidogo vya bahari ambavyo viko hatarini kuathiriwa bila kuwepo na mikakati ya uhifadhi.

Katika kuhakisha ushiriki wa wananchi wenyeji katika utekelezaji wa mradi huo na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari tayari kazi za kuwajumuisha wananchi wa vijiji vy karibu na Ras Mkumbuu katika mipango ya utekelezaji zimeanza kwa kusikiliza maoni ya wanachi juu yamiradi wanayopenda ianzishwe ili kuwasaidia kuboresha huduma za kijamii, kukuza uchumi na kupunguza shindikizo kwa matumizi ya rasilimali za bahari.

Mwishoni mwa wiki iliyopita Meneja wa Taasisi ya EcoAfrica Environmental Consultants (Tanzania) - Frida Lanshammar ambayo ndiyo iliyohusika na upembuzi yakinifu wa mradi ASCLME alifanya ziara katika Vijiji vilivyo jirani vya Wesha Shehia ya Wesha na Ndagoni, Shehia ya Ndagoni Wilaya y a Chake Chake kujadiliana na wananchi wa huko juu ya jinsi wananvyo weza kufaidika na mradi huo.

Meneja huyo alisema wananchi wa vijiji hivyo kupitia kamati zao za maendeleo wamechagua kuanzishiwa vituo viwili vikubwa vya maendeleo ya kijamii(kimoja katika kila shehia) vitakavyojumuisha ndani yake huduma muhimu za kijamii na kiuchumi zinazohitajiwa na wanaanchi wa hapo.

Meneja Frida amezitaja baadhi ya huduma ambazo zimebainishwa na wanachi wa huko kama vipaumbele vinavyotakiwa kuwemo katika vituo hivyo vya maendeleo ya kijamii kuwa ni huduma za kumbi za mikutano, ofisi ya shughuli za kitalii, darasa la kisomo cha watu wazima, chumba cha computer na Internet. Huduma nyengine ni soko la kuuzia mboga mboga na matunda, sehemu yakukaushia mazao ya baharini na matunda, vyoo na sehemu maalum kwaajili ya huduma ya Afya.

Frida amesema hata hivyo bado ni mapema mno kuzungumzia gharama halisi za ujenzi wa vituo hivyo ambavyo ufadhili wake utakuwa nje ya mradi mkubwa na iwapo ujenzi wake utajumuisha kila kitu ambacho wananchi wa vijiji hivyo wamechaguwa kujumuishwa kwa vile itategemea zaidi mhisani ataejitokeza kuufadhili ujenzi wa vituo hivyo vya kijamii.

Hata hivyo katika hatua za awali tayari shirika la maendeleo la Denmark DANIDA limeonesha nia ya kufadhili ujenzi wa vituo hivyo na tayari kwa kuanzia limekuwa mstari wa mbele katika kugharamia mchakato mzima wa kupata maoni ya wananchi juu vituo vya maendeleo ya kijamii na kusaidia pia upatikanaji wa michoro ya ujenzi .

Katika ziara ya hivi karibuni ambayo ilifadhiliwa pia na shirika la maendeleo la Denmark DANIDA wananchi wa vijiji vya Ndagoni na Wesha walifanikiwa kushirikiana na Mtaalamu wa Michoro na Usanifu majenzi kutoka Afrika Kusini Profesa K. Barker kuchaguwa maeneo ya Skuli ya Wesha na Skuli ya Ndagoni kuwa yanaweza kutumika kujenga vituo hivyo vya kijamii

Sheha Kahatan, mkaazi wa Shehia ya Ndagoni na mjumbe wakamati ya maendeleo ya shehia hiyo amesema kuwepo kwa vituo vya aina hiyo imekuwa ni ndoto yao ya siku nyingi na kupatikana kwa fursa hiyo kutawasaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na umasikini wa kipato na kuimarika kwa huduma za kijamii kijijini kwao.

Mwanakijiji huyo amesema wao kilio chao kikubwa katika shehia ya Ndagoni ni kupatikana kwa huduma za afya katika kituo hicho na kuwaondoshea tatizo la sasa ambapo wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita nne hadi kituo cha Afya cha Wesha kufuata hata huduma ndogo tu za kufunga vidonda.

MWISHO

MARPS Zanzibar

VIONGOZI WA DINI WAAHIDI KUSAIDIA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI YA HIV MIONGONI MWA MARPS ZANZIBAR
Na Ali Haji Hamad, Pemba Press Club
Viongozi wa dini wameahidi kila mmoja kwa nafasi yake kuendelezeza jitihada za kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU na UKIMWI miongoni mwa makundi hatarishi (MARPS) Zanzibar.
Wakizungumza katika mkutano wa kutathmini Utendaji wa jumuiya ya taasisi za kidini ya Maendeleo na Mapambano ya Ukimwi Zanzibar (ZIADA) wanadini hao wamesema japo matendo yanayofanywa na kundi hilo ambalo linajumuisha watumiaji wa madawa ya kulevya, wanaume wanaufanya mapenzi na wanaume wenzao (mashoga) na wafanyaji wa biashara ya ukahaba hayakubaliki katika dini hizo lakini bado viongozi wa dini wanawajibu wa kuwanusuru na kuwaelekeza katika mwenendo unaokubalika.
“Tusiwatenge tuwaweke karibu, tuwaelekeze madhara ya matendo wanayoyafanya kwa maisha yao ya dunia na maisha yao ya baadae akhera nadhani hiyo ndiyo njia bora ya kuyasaidia makundi haya hatarishi” alisema bi Bi Ramla Salim wa Skuli ya Kiislamu Kizimbani alipokuwa akichangia mjadala huo.
Naye ustadhi Muhammed Massoud Said wa msikiti wa Vijana Wete alielezea kusikitishwa kwake na tabia ya viongozi wa dini ya kuyapuuza moja kwa moja makundi hayo kama vile wao si sehemu ya jamii. “Tumekuwa tukiyapuuza makundi hayo, hatutaki kuonana nao, kuzungumza nao wala kuwafikia katika harakati zetu tunazofanya, hata tukikutana nao barabarani kwa bahati mbaya tunageuza uso tusiwaone.
Hili si jambo jema na nadhani tukifanya hivi tutakuwa bado hatujawasidia” alsema ustadhi Muhammed Akielezea ubaya wa kuyapuuza makundi hayo ustadhi Muhammed alisema yakiendelea kuachwa bila kufanyiwa mkakati wa kuyasaidia, matendo mabaya wanayoyafanya yanaweza kukua na kutapakaa na madhara yake kuingia katika jamii nzima kwa vile bado makundi hayo ni sehemu ya jamii ya Wazanzibari na maisha yao ya kila siku yana mwingiliano wa moja kwa moja na maisha ya watu wengine wa kawaida.
Hata hivyo baadhi ya viongozi waliohudhuria walielezea wasi wasi wao kuhusu jinsi ya kuyafikia makundi hatarishi kwa vile njia zinazotumiwa sasa na viongozi wa dini kutowa elimu ya VVU na UKIMWI kama vile hotuba katika sala za Ijumaa, mihadhara na madrassa haziwagusi moja kwa moja watu hao.
“Jambo moja la kukumbuka ni kwamba hapa tunazungumzia watumiaji wa madawa ya kulevya, wafanyaji wa biashara ya ukahaba na mashoga na hawa hawahudhirii misikitini, hawajitokeze kwenye mawaidha wala hawaendi Madrassa jee tutatumia njia gani ili kwafikia” alitoa changamoto Dr. Issa Ziddi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Utafititi wa Integrated Behavioral and Biological Surveillance Survey (IBBSS) uliofanywa na Kitengo cha Kudhibiti Ukimwi Zanzibar (ZACP) mwaka 2007 kiwango cha maambukizi miongoni mwa watumiaji wa Madawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga sindano (IDU) ni asilimia 16.0, kiwango cha maambukizi miongoni mwa wanawake wanaofanya biashara ya ukahaba (CSW) ni asilimia 10.8 na miongoni mwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao(MSM) ni asilimia 12.3 tofauti na kiwango jumla cha maambukizi kwa jamii ambacho kipo chini ya asilimia moja (asilimia 0.6).
Mapema bwana Nuhu Salanya, mwakilishi wa kanisa la Anglican katika jumuiya ya ZIADA aliwataka viongozi wa dini wasiogope kukubaliana na watu wanaofanya matendo maovu katika jamii kwa sababu hiyo ndio kazi yao.
“Kazi yetu kama viongozi wa dini ni kushughulikia matatizo ya kitabia miongoni mwa wafuasi wetu na kushawishi mabadiliko chanya kwa matendo hayo kupitia imani za kiroho” alisema Bw. Salanya .
Mapema wajumbe waliohudhuria mkutano kama huo katika ukumbi wa uwanja wa Gombani wetu wamepata moyo kuona kuwa harakati wanazoziendeleza kupitia misikiti, madrassa mihadhara na mikusanyiko ya kiajamii zimeanza kuzaa matunda ikiwa ni pamojana kudhibiti kasi ya maambukizi nakuifanya ibakishe chini ya asilimia moja (0.6) kwa zaidi yamiaka mitatu. mwisho