MAKAAZI HOLELA YA MILIMANI YANAVYOLITATIZA JIJI LA
MWANZA. (Makala hii niliichapisha kwa
mara ya kwanza katika gazeti la nipe habari mwezi August 2011)
Na Ali Haji
Hamad, Mwanza
- ·
Yanaendelea
kukua
- ·
Kuyarasimisha
haiwezekani
- ·
Kuyaacha yalivyo
yanatia kichefu chefu
- ·
Huduma za usafi
wa maji taka na taka ngumu zinakwama
- ·
Hakuna bajeti
iliyotengwa kushughulikia
Si siri kwamba
Mwanza ni miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi nchini Tanzania Ukuaji huo
unaonekana takriban katika Nyanja zote zikiwemo zile za kiuchumi na kijamii.
Wanaotembelea Mwanza watakuwa ni mashahidi wa ongezeko la ukuaji katika biashara
za magari, mabenki, mahoteli, na biashara za kati na kati za maduka. Aidha
ongezeko la Idadi ya watu nalo ni dhahiri. Wingi wa watu huonekana sio tu kwa
idadi kubwa ya wale wanaokwenda na kurudi katika mitaa ya jiji hilo bali pia
katika utafutaji huduma kama vile za kiafya, ulipaji wa bili za maji na umeme
na foleni ndefu katika mabenki.
Takwimu nazo zinaonesha hivyo. Idadi ya watu
Mwanza sasa inakisiwa kuwa 1,269,257 kutoka 1,200,000 mwaka 2010. Katika sensa
ya watu na makazi ya mwaka 2002 idadi ilikuwa 476,646. Wakati huo ongezeko la
kimaumbile lilikuwa asilimia 3.2 na kasi ya uhamiaji mijini ilikisiwa kuwa
asilimia 8.
Ni faraja pia kwamba hata sura ya mji wenyewe
nayo imebadilika. Kwa wale waliolipa kisogo jiji hili katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita na kurejea tena hivi karibuni kama mimi, hawatakosa kuvutiwa
na sura ya mabadiliko ambayo yamekuwa yakitokea. Barabara nzuri za katika kati
ya jiji, magorofa mapya yaliyomalizika na yanayoendelea kujengwa, bustani nzuri
katika baraba bara za Nyerere na mzunguko
(round about) wa samaki katika barabara ya Kenyata ni miongoni mwa mambo
yanayolipa jiji hilo sura ya matumaini.
Hata hivyo nyuma
ya sura hii ya matumaini ya jiji la
Mwanza kuna sura mbaya na ya chukizo inayoweza kumfanya mtu asahau uzuri wote
niliokuwa nimeudokeza hapo awali. Chukizo hili si jengine bali ni lile
linalotokana na makaazi holela ya milimani. Makaazi haya yametapakaa tokea
kandokando ya jiji hilo katika milima ya Mkolani, Mahina, na Kirumba hadi
katikati ya jiji lenyewe katika milima ya Igogo, Seketure na Bugando. Kwa
mujibu wa utafiti wa mabadiliko na mageuzi katika serikali za mitaa uliofanywa
na Siri Lange wa taasisi ya Chr. Mischelsen kwa kushirikiana na taasisi ya
Utafiti juu ya Umasikini ya Tanzanaia (REPOA) makaazi hayo holela yamo takriban
katika vilima 14 vya mji huo.
Japo inaweza
kuonekana kuwa makaazi holela si jambo geni kwa jiji kama Mwanza ambalo zaidi
ya asilimia 70 (makaazi 49000) ya makaazi (65,500) ya jiji hilo hayakupimwa
lakini hili la makaazi ya milimani lina uzito wa kipekee. Kwanza ni kutokana na
nafasi (position) ya milima hiyo katika sura ya jiji la Mwanza. Kwa mfano
milima ya Igogo ipo katikati mno ya Mwanza kiasi kwamba kuendelea kubakia
katika sura yake hiyo itaendelea kuwa sawa na doa jeusi katika shati jeupe hata
kama maeneo mengine ya mji yatapendezeshwa kiasi gani.
Pili makaazi ya
milimani yanahitaji mtazamo wa kipekee kutokana na umuhimu wa maeneo hayo kwa
mazingira na usafi wa jiji. Usafi wowote utakaofanywa katika mji wa Mwanza na
kupuuza maeneo hayo itakuwa ni sawa na kuweka maji kwenye pakacha kwa sababu
uchafu utakaopuuzwa milimani ni rahisi kushuka wenyewe ama kushushwa na mvua
kuja maeneo ya chini na pengine kwenye ziwa ambalo ni chanzo kikuu cha maji
yanayotumiwa majumbani katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera.
Tatu makaazi ya
milimani yanahitaji mtazamo wa kipekee kutokana na kuwepo na hadithi za miaka
mingi za kulishughulikia tatizo la makaazi holela ya huko ambazo hadi
tunaandika makala hii hazijaleta mafanikio.
Hadithi za kutafuta suluhisho
Kwa uchache
hadithi za kutafuta suluhisho la makaazi holela katika makaazi ya milimani
ya jiji la Mwanza lina miaka isiyopungua
12. Zilianzia mwishoni mwa miaka ya 1998
wakati serikali ya Tanzania ilipoamua kupanua katika manispaa mradi uliokuwa
umeanzia Dar es salaam wa Sustainable City Programme ikiwa ni sehemu ya miradi
kadhaa ya aina hiyo chini ya Umoja wa Mataifa. Mwanza ikiwa manispaa wakati huo
ilianzisha mpango wake uliojulikana kwa jina la Sustainable Mwanza Programme.
Mradi huo baadaye ulibadilishwa jina na kuitwa Capacity Building for
Environmental Management (CBEM) baada ya kupata ufadhili wa shirika la
maendeleo la Denmark DANIDA wa dola za kimarekani 1.9 milioni ambazo ni takriban
shilingi za Tanzania bilioni tatu. Mradi
huo ulioishia mwaka 2003 ulilenga kulijengea uwezo jiji la Mwanza wa
kushughulikia mazingira ya jiji hilo ikiwemo mifumo ya maji taka, taka ngumu na
kuboresha miundo mbinu ya kimazingira katika makaazi holela. Kumbu kumbu pekee iliyoachwa na mradi huo kwa
watu wa kawaida ni zile bara bara za miguu zilizojengwa katika wadi za Igogo na
Pamba ambazo mwendelezo wake uliisha wakati mradi ulipoisha.
Kiongozi mmoja
wa jumuiya ya kihabari iliyoshiriki kwa karibu wakati wa utekelezaji wa mradi
huu aliniambia kuwa mpango ulikuwa ni pamoja na kuhamisha makaazi holela na kwa
wkati huo yalikuwa ni 35000 na yalihitaji shilingi za Tanzania 50 bilioni. Sasa
kwa mujibu wa takwimu za 2008 za jiji laMwanza kuna makaazi 65,500 na
kulishughulikia tatizo lake inahitaji shilingi Billioni 200 kwa mujibu wa
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe.
Wakati mradi wa
CBEM ukiendelea mwezi April 2001 Shirika la Maendeleo la Denmark Danida
lilizindua mradi mwingine uliojulikana kama Sustainable Development Programme
in Mwanza uliokuwa na madhumuni matatu. Kwanza kuboresha mazingira ya makaazi holela
kwa mujibu wa vigenzo vya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Makaazi
UN-HABITAT. Pili ni kuzijengea uwezo CBOs na NGOs ziweze kusaidia kazi hiyo.
Tatu ni kusaidia upatikanaji wa haki za kisheria za watu waishio katika makaazi
holela ya milimani.
Kwa kuanzia
mradi ulikuwa umezilenga kaya 2,500. Wananchi walishirikishwa katika kuchagua
mahala pa kupitisha barabara na maeneo ambayo yangeweza kuanzishwa vituo vya
afya na kujengwa shule. DANIDA kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi na Upimaji (UCLAS) walikuwa na kazi ya kupima
maeneo na kuetengeneza ramani ili kufahamu maeneo yatayotumika na nyumba ambazo
zingestahiki kubomolewa. Wananchi walitakiwa kuchangia shilingi 20,000 kila kaya
kusaidia zoezi hilo kendelea na ili
kuwafanya walione ni la kwao.
Hakuna hasa
anaejua kilichotokea pale mwezi Agosti 2002 DANIDA walipotangaza kujitoa katika
mradi huo na wakaondoa pia shilingi milioni 200 zilizokuwa zimetengwa kwa hatua
ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo. Hivyo hadithi nyengine ya kutafuta
suluhisho la makaazi holela nayo ikaishia patupu huku wale wanaolitakia mema
jiji la Mwanza wakiwa hawajui kilichotokea. Inavyoonekana si
wananchi wa kawaida tu ambao hawajui kwanini mipango ya kutafuta suluhisho kwa
tatizo la makaazi holela ya milimani zinaishia kuwa hadithi za paukwa pakawa
bali hata Mstahiki Meya wa jiji la Mwanza Josephat Manyerere. Nilipomuuliza
kuhusu kinachokwamisha mipango mbali mbali ya kushughulikia tatizo la makaazi
holela ya milimani katika jiji la Mwanza
alisema yeye hafahamu kuhusu uwepo wala utekelezaji wa mipango hiyo na
anahitaji kufanya utafiti kwanza.
“Unajua sisi
tumekuwepo madarakani kwa miezi minane tu na hatufahamu mambo hayo
yaliyofanyika nyuma. Wewe mwandishi nenda tu sisi tutafanya utafiti tukiwa
tayari tutakuita” aliniambia Meya huyo ambae pia ni diwani wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Ni zaidi ya miaka
10 imepita tokea mradi wa kurkebisha makaazi ya Milimani ulipofeli na makazi ya
milimani sio tu kwamba hayajaboreshwa bali pia yamekuwa yakiongezeka na
kuifanya hali kuwa ngumu zaidi. Suala kubwa ambalo mtu anaweza kujiuliza kwa
sasa jee ni ipi hali ya Makaazi ya milima na hatima yake ni ipi? Je sasa ni ruksa au imeshindikana tu
kushughulikiwa? Na ni wapi zilipoishia hadithi za kulishughulikia tatizo hili?
‘Ruksa’ kukaa Milimani Mwanza
Kwa viongozi wa
jiji la Mwanza unapowauliza iwapo makaazi holela ya milimani sasa yamepata
baraka, ama ni “ruksa” kuwepo, huwa wanapata kigugumizi kutowa jawabu la moja
kwa moja lakini si kwa afisa maendeleo ya jamii wa mkoa wa mwanza, Isaac Ndasa.
Bwana Ndasa yeye aliniambia mabadiliko ninayoyaona katika makaazi ya milimani Mwanza
si ongezeko la makaazi bali ni dhana juu ya makaazi yenyewe.
“Dhana ya zamani
ilikuwa kukaa milimani ni haramu lakini dhana ya sasa ni kwamba kukaa milimani
si tatizo ikiwa mtu atafuata taratibu za huko” alisema afisa huyo na kuongeza
kwamba inawezekana hiyo ndio sababu ya kuonekana kwamba makaazi ya huko
yanakua.
Huu unaweza
kutafsiriwa kwamba ni msimamo wa afisi yake lakini ushahidi unaonesha kuwa ni
msimamo pia wa afisi za wengine wanaoogopa kusema wazi wazi kama vile afisi ya
jiji la Mwanza..Kwa mfano mtu wa
kawaida anapoona jitihada za kufikisha miundo mbinu ya umeme na maji huko japo
kwa wateule wachache wenye uwezo katika wakati ambao watu walitarajia kuona
mikakati ya kuhama au kuhamishwa ni ishara kwamba labda sasa makaazi hayo
holela yameanza kupata baraka. Hata ule ukimya tu juu ya ujenzi wa makaazi
mapya huko mengi yao yakiwa ya chumba kimoja au viwili nayo ni ishara nyingine
kwamba labda sasa ni ruksa.

Kwa vyovyote
itakavyokuwa watu wanaofuatilia tatizo hili la makaazi holela ya milima ya Mwanza
akiwemo Mlagiri Kopoka wa Nyakato wanauchukulia msimamo kwamba makaazi ya milima ni ruksa
ulioelezwa na Afisa maendeleo jamii ywa mkoa wa Mwanza na ule usioelezwa wazi
na jiji kuwa ni msimamo uliotokana na kukata tamaa au wa kujikosha baada ya
ahadi kadhaa za kwamba tatizo hilo linashughulikiwa kuishia patupu. Kwa mfano, mbali
na jaribio la kushughulikia tatizo la makaazi holela ya milimani nililolitaja
hapo awali la mwaka 2001 ambalo halikufanikiwa kulikuwa na jaribio lingine pia
mwaka 2002. Afisa wa Mipango miji ambae pia ni Mratibu wa mpango wa
urasimishaji makaazi mwanza Maduhu Kazi, aliliambia gazeti hili kwamba katika
mwaka huo manispaa ya Jiji La Mwanza ilitoa namba za nyumba kwa wakaazi wote wa
huko ili kuwatambua lakini baadae hakuna kilichoendelea.
Mwaka 2005 jiji
pia lilipiga picha za angani za makaazi yote ya milimani ili kupata picha
halisi ya maeneo ya huko na baadae kufuatiwa na tamko la mkurugenzi wa jiji ya
kuwataka wakaazi wa huko wahame na wahamie katika maeneo mengine lakini hakuna
aliyehama.
Mwaka 2008
wakati naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dk. Asha Rose Migiro alipotembelea
jiji la Mwanza na kuonana na Mkurugenzi wa jiji hilo Wilson Kabwe ambae ndie
mkurugenzi wa sasa. Vyombo vya habari vilimkariri Mkurugenzi huyo akimueleza
Dk. Migiro kwamba wameanza kuboresha maeneo ya milimani kwa kutengeneza michoro
ya kuboresha makaazi hayo yakiwemo ya Mkolani na Kiloleni na akasema
watakaohamishwa watapelekwa katika viwanja 5,000 vilivyokwisha pimwa kwa kazi
hiyo.
Mkurugeni huyo
hakuwahi kukanusha kauli hiyo hapo kabla hadi nilipomuuliza utekelezaji wa
mpango huo hivi karibuni. Alisema yeye hakuwahi kutowa kauli hiyo na anachoweza
kusema ni kwamba kuna viwanja 6,000 vimepimwa kwa ajili ya kuboresha makaazi Mwanza
na si kwa watu wa milimani pekee. Nilipomuuliza maeneo vilipo viwanja hivyo
aliniambia:
“Si muhimu kujua viwanja viko maeneo gani wewe jua tu kwamba kuna
viwanja 6,000 vimepimwa kuboresha makaazi”
Afisa Mipango
miji wa jiji la Mwanza Maduhu Kazi nae aliniambia kwa kadri anavyofahamu hakuna
viwanja 5000 vilivyotengwa kwa ajili ya wakaazi wa milimani. Alisema jiji
limekuwa katika harakati za kupima viwanja kwa ajili ya watu wote. Alifafanua
kuwa katika utekelezaji wa hilo wao wanaendesha mradi unaojulikana kama mradi
wa viwanja 3,500 na tayari wamefanikiwa kupima kupitia mradi huo jumla ya viwanja
1,700. Hata hivyo hakuna vyovyote katika viwanja hivyo vilivyokusuduwa watu
wataohama au kuhamishwa kutoka makaazi holela ya Milimani. “Hivi ni viwanja kwa
ajili ya kila mtu, si vya wakaazi wa milimani” alisisitiza afisa huyo.
Majaribio
mengine ya hivi karibuni ambayo mtu angedhani ulikuwa ukombozi muafaka kwa
makaazi holela ya Milimani ni mradi wa kupanga upya makaazi (urasimishaji)
uliofadhiliwa na Wizara ya Ardhi na Mradi uliolenga kupata usaidizi wa UN-HABITAT
kuboresha makaazi holela katika milima ya Mwanza.
Urasimishaji Makaazi
Kuhusu Mradi wa
kurasimisha makaazi ambao umeanza tokea mwaka 2009 jiji la Mwanza lilipanga
kurasimisha makaazi 15,000 na kusajili 45000 pamoja na kuyapatia hati kwa
kipindi cha miaka miwili kupitia mradi huo wenye thamani ya shilingi 1.6
bilioni ambapo hadi sasa wamefanikiwa kurasimisha makaazi 10,333.
Afisa mipango wa
jiji la Mwanza alisema hata hivyo urasimishaji huo ambao hufanywa kwa
kutengeneza upya ramani za maeneo husika, kupima viwanja na kutoa hati na
kuweka barabara za ndani ya mitaa hata hivyo hautoyahusisha maeneo ya milimani
kwa vile yanakatazwa kwa mujibu wa sera ya mipango miji ya mwaka 2007 na sheria
ya ardhi ya 1999.
Afisa huyo akitoa
ufafanuzi alitaja sababu tatu ambazo zinapelekea maeneo ya milimani kuachwa katika
mpango wa urasimishaji kwamba kwanza ni kutokana na Sera ya mipango miji ya mwaka 2007 ambayo
ndiyo iliyoandika utaratibu wa urasimishaji makaazi imekataza kurasimisha
maeneo ya milimani, mabondeni na maeneo yaliyokwisha pimwa. Pili alisema
urasimishwaji hautofanywa katika makaazi holela ya milimani kwa sababu zoezi
hilo linaweza kupelekea kubomolewa kwa baadhi ya makaazi jambo ambalo ni
kinyume na maelekezo ya mradi wenyewe. Na sababu ya tatu Maduhu alisema ni
kutokana na ukweli kwamba ni vigumu katika maeneo ya milimani kupata ardhi
inayokubalika kisheria kurasimisha.

Alisema wakati
katika maeneo ya kawaida eneo la chini linalokubalika kurasimishwa ni mita za
mraba 120 katika eneo la milimani kiasi cha mita za mraba 300 zinahitajika.
Alisema hiyo ni kutokana na ukweli kwamba katika eneo la milimani panahitajika
pia papatikane eneo la kupanda miti ili kuzuia mmong’onyoko na eneo la kutosha
kuchimba makari ya maji machafu na vyoo.
Mradi ulioota Mbawa
Ama kuhusu mradi
wa UN HABITAT huu ulikuwa ni mradi wa ushirikiano kati ya jiji la Mwanza na
Shirika la Umoja wa mataifa linashoghulikia makaazi la UN HABITAT. Mradi huu
ulilenga kuimarisha miundombinu katika mkaazi hayo ya milimani na kuwapatia
fursa ya kuhama na kuhamia mahala pengine wale ambao wangependa kuhama. Hata
hivyo licha ya Mkurugenzi wa jiji la Mwanza Wilson Kabwe kukaririwa na vyombo
vya habari akimueleza Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Dk. Asha Rose
Migiro mwaka 2008 kuwa andiko la Mradi lilikuwa tayari miaka mitatu baadae
(hadi 2011) bado hakuna dalili zozote za kuwepo kwa mradi huo.
Nilipoomba
ufafanuzi kuhusu mradi huo Mkurugenzi huyo alisema
“Ile ( UN –HABITAT) ni
taasisi ya kimataifa. Mchakato wake unachukua muda mrefu, wakiwa tayari wewe
utaona”.
Kauli Hewa
Wakati ‘mishemishe’
hizo za kuwafanya wanaharakati wa mazingira, watetezi wa haki za binaadamu na
wananchi kwa jumla waone kwamba kuna jitihada za kulishughulikia tatizo la
makaazi holela ya milimani zikiibuka na kufifia miaka nenda miaka rudi
imebainika kuwa sehemu kubwa ya kauli zilizokuwa
zikitolewa na Manispaa ya jiji la Mwanza zilikuwa ni kauli za midomoni zaidi
kuliko za kitaalamu na mara nyingi zilitolewa kukidhi mahitaji ya wakati. Kwa mfano wakati
jiji likizungumzia kuwahamisha watu na kuwapeleka mahala pengine halijawahi kutenga
wala kupima viwanja kwa ajili ya kuwahamishia watu hao wala kuweka fedha katika
bajeti kwa kufanikisha zoezi hilo.
Hapakuwahi
kuwepo na bajeti ya jiji ya kulishughulikia tatizo hilo katika miaka iliyopita
na hakuna bajeti ya kulishughulikia tatizo hili katika mwaka huu wa fedha 2011/2012
kwa mujibu wa Meya wa jiji la Mwanza Bwana Josephat Manyere na Mkurugenzi wa
jiji Wilson Kabwe.
Matata Henry
Matata Mwenyekiti wa kamati ya Mipango ya jiji la Mwanza ambae pia ni Diwani wa
Kata ya Kitangiri (CHADEMA) yeye alisema tatizo la makaazi holela ya milimani
ni kubwa na ni vigumu kushughulikiwa kwa bajeti ya jiji
“Labda kama zipatikane
serikali zenye pesa zao zisaidie”.
Mbali na
kutokutengewa bajeti tatizo hilo pia halijaandaliwa mpango wowote wa uhakika wa
muda mfupi, muda wakati au muda mrefu kulishughulikia hata katika wakati huu
ambapo serikali ya Halmashauri ya jiji la Mwanza inaongozwa na Chama cha
Upinzani cha CHADEMA. Nilipomuuliza Meya wa Jiji la Mwanza kwamba wao wakiwa ndio
wanoshikilia usukani wanamipango gani kuhusiana na tatizo hilo alisema
hawakuingia na mkakati wowote kuhusu makaazi holela ya milimani.
“Hili jambo si
la mtu mmoja huwezi kuwa na mikakati juu ya jambo kama hili ni mpaka uwasikilize
wenzio wanasemaje”
Labda kukosekana
huku kwa mipango ya dhati ya kulishughulikia tatizo hili kumetokana na ukweli
kwamba bado uongozi wa juu wa jiji la mwanza haujakubali kwa dhati kwamba
makaazi holela ya milimani ni tatizo.
Nilipomuuliza Mkurugenzi
wa jiji Wilson Kabwe anaichukuliaje hali ya makaazi holela ya milimani
alinijibu kwa kuniuliza suali pia:
“Wewe umeona hizi ndio squatters?” “Haya ni
makaazi tu. Hayajapangiliwa vyema basi” alisema na kuendelea kuhoji: “Wewe
umewahi kuona squatters za wapi. Hebu nenda Kibera (Nairobi), nenda na Zaire
(CapeTown) uone. Watu wanatembea zaidi ya kilomita moja huko kufuata vyoo vya
maboksi vilivyowekwa barabarani” alisema
Alisema haoni
kwamba hali ni mbaya katika makaazi hayo ya milimani kama watu wanavyopenda
kusema. Alisema japo watu wana vyoo vibovu lakini wanavyo tofauti na sehemu
nyengine na akasisitiza kwamba hali ni bora kuliko maeneo mengine.
Hata hivyo mama
Mashaka mmoja wa wakaazi wa milimani katika milima ya Igogo alisema hajawahi
kuwaona viongozi wa jiji wakitembea huko zaidi ya wale wanaokwenda mara moja kwa
mwaka kudai kodi za viwanja za shilingi 10,000/=.
Maisha Milimani
Pamoja na
Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Wilson Kabwe kudhani kwamba makaazi holela ya milimani Mwanza si tatizo
sana kwa sababu tu hayajafikia viwango vya Kibera (Nairobi) na Zaire (CapeTown)
hali ya maisha na huduma za kijamii milimani kwenyewe inaeleza tofauti.

Katika ziara
ndefu ya kutemblea milima ya Mkolani Igogo, Bugando, Mkuyuni na Mahina
nilishuhudia mambo kadhaa ya kuthibitisha adha na hali ya kukatisha tamaa ya
huko. Mojawapo ya mambo hayo ni ulemavu wa mzee Hoza (57) mkaazi wa milima ya
Igogo. Kwa mujibu wa maelezo ya mama Betty, mke wa Mzee Hoza, baba huyo amepata
ulemavu wa kudumu baada ya kuvunjika mgongo alipoanguka wakati akitembea katika
vigingi vya vichochoro vya huko kwenda mjini miezi sita iliyopita. Kwa sasa
mzee Hoza hawezi kusimama wala kukaa. Baiskeli ya magurudumu matatu nilioishuhudia
hapo mke wake aliniambia ilitafutwa imsaidie lakini haijamsaidia sana kwa
sababu hapana mahala popote anapoweza kuiendesha baiskeli hiyo zaidi ya ndani
ya boma la nyumba yao ambayo uwanja wake upana na urefu wake hauzidi mita 3.
Mama Betty alinieleza kuwa kwa sasa kigari hicho hutumika tu kumtolea kitandani
na kumpeleka ukumbini kuoga na kumrejesha kitandani.
Mama Betty
alieleza kuwa hali ilikuwa ngumu zaidi katika siku za awali ambapo Mzee Hoza mara kwa mara alikuwa akihitaji
kupelekwa Hospitali ya Bugando. Anasema walikuwa wanalazimika kumbeba kwa
mikono masafa marefu katika mahala ambapo hata vichochoro vya kupita naye navyo
ni shida.
Ubovu wa njia
hata za kutembea kwa miguu ambao ni chanzo cha ulemavu wa kudumu wa Mzee Hoza
ni moja tu ya adha zinazowakumba wakazi wa Milimani.
Mambo mengine
ambayo hayawezi kufichika hata kwa mtu atakayetembea siku moja tu katika
makaazi Holela ya milimani ni kuzagaa kwa maji machafu yanayotirirka kutoka
majumbani na makaro yaliyopasuka. Uchache na ubovu wa vyoo, kukosekana kwa
mifumo ya kuhifadhi taka ngumu, ukosefu wa miundo mbinu ya maji taka, shida ya
maji na nyumba chache tu zenye umeme. Hali ya kukuta karo ya choo pembeni ya
dirisha la mtu mwingine au kibanda cha choo mbele ya nyumba ni ya kawaida.
Mama mmoja aliyejitambulisha
kwa jina la Mama Mashaka alituambia watu wa milimani sio tu kwamba wanategemea
vyoo ambavyo ni vibovu na vyengine vimejaa lakini kuna kundi kubwa pia halina
hata hivyo vyoo. Alituambia kundi hili hujisaidia kwenye mifuko ya plastiki na
kutupa vinyesi hivyo mahala popote watapojaliwa.
“Hapo uliposimama
hapo ndugu mtangazaji usingeweza kufika leo kama si kelele zangu ninazopiga
kila siku. Hujisaidia kwenye mifuko na kutupa uchafu wao kila mahala mpaka hapa
nyumbani kwangu” aliniambia mama mashaka.
Mama huyo
aliendelea kueleza kuwa mbali na tafrani ya watu kuishi bila vyoo hata wale
walionavyo nao wana tatizo kwamba vyoo vyao vinapojaa hawana jinsi ya
kuvitapisha. Watu hawa husubiri mvua inaponyesha na kutiririsha uchafu wao pamoja na maji ya mvua jambo ambalo alisema
linatishia afya zao. Mama Mashaka alilaumu jiji la Mwanza kwamba wanachofanya
ni kukusanya tu shilingi 10,000/= lakini hakuna huduma watowayo.
Tatizo la ugumu
wa kusafisha maji taka lilizungumziwa pia na Msaidizi meneja uhusiano wa
mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (MWAUWASA) Mwanza, Robert Masunya. Meneja
huyo alisema hali mbovu ya ukosefu wa miundo mbinu ndio kikwazo kikubwa.
Alisema kwa hali
ilivyo sasa hakuna njia yoyote ya kufikisha bomba la maji taka katika maeneo ya
milima kama ya Igogo wala njia ya kufikisha gari la kufyonza maji taka.
“Kama gari
linafika isingekuwa tatizo. Tuna magari ya kutosha hapa kwa ajili ya kazi hiyo"
Masunya nae alilaumu pia uongozi wa jiji la Mwanza kwamba haujafanya jitihada
za kutosha kurekebisha hali mbaya ya huko. Amesema hali hiyo inakuwa kikwazo
kwa mipango ya MWAUWASA ya kudhibiti maji taka.
Pamoja na tatizo
la maji taka wakaazi wa milimani wanakabiliwa pia na tatizo la kutupa taka
ngumu. Katika ziara ya milimani iliyofanywa na mwandishi wa makala hii hakuwahi
kushuhudia kontena lolote lililowekwa mahala kwa ajili ya kuhifadhi taka ngumu.
Hata lile dogo lenye ukubwa wa ndoo ya plastiki ambalo lingeweza kuwekwa
upenuni kwa nyumba halionekani popote.
Mama mashaka
anasema wanapowauliza watu wa jiji kuhusu mahala pa kutupa taka ngumu
huwaelekeza waende kutupa taka hizo katika kontena la sokoni. Kutoka milima ya
Igogo anapoishi mama mashaka na Sokoni anakoelekezwa kutupa takataka ni umbali
wa zaidi ya nusu kilomita.
“Hebu weye
mtangazaji ona na miguu yangu hii mibovu halafu niende kutupa taka sokoni. Mi
siwezi, natupa tu popote kama wanavyofanya wenzangu” alisema akionesha miguu
yake aliyokua ameifunika kitenge.
Hali hii mbaya
ya mazingira inazidisha tishio la milipuko kwa wakaazi wa milimani. Wakaazi wa
huko akiwemo mama Mashaka analijua hilo. Yeye anadai jiji halitaki kuwasaidia
ndio maana kila linapotokea tatizo wao ndio wa mwanzo huko kuathirika.
Hayo ni mbali ya
ugumu wa kufikisha huduma muhimu za dharurua kama vile za zimamoto ama gari la
kubebea wagonjwa pale linapotokea la kutokea.
Ikiwa wewe ni
muumini pia wa haki za watoto na unadhani pia watoto wana haki ya kucheza, pengine
wawe na kijiwanja kidogo hivi cha kucheza mpira au hata kufukuzana tu wenyewe
na kufurahi basi haki hiyo haipatikani. Wenyewe hukaa tu juu ya majabali na
kushangaa wale wageni wachache wanaofika huko ama kuangalia gari zipitazo barabarani
na mara nyingine mitumbwi ieleayo ziwa Victoria.
Hata hivyo
katikati ya adha hizi zinazowakumba wenyeji wa makaazi holela ya milimani bado
kuna jambo moja zuri linalowafanya kutabasamu. Jambo hilo si jingine bali ni
upendo na ujirani mwema miongoni mwao.
Bi Sophia John
aliniambia kuwa watu wanaoishi milimani wanapendana sana kwa sababu kila mmoja
anamuhitaji mwenziwe.
“Huku hata ukiwa
na mgonjwa tu basi huwezi kumfikisha barabarani peke yako ni lazima upate
msaada wa majirani. Hili linatufanya tuwe kitu kimoja” alisema Bi Sophia.
Hata hivyo
pamoja na kuishi kwa upendo nilipowauliza kuhusu uwezekano wa kuhama na kuhamia
mahala pengine wengi wao walionesha utayari wa kufanya hivyo. Mmoja wao ni mama
Mama Betty amabae wamekaa huko yeye na mumewe na watoto wao kwa zaidi ya miaka
30 sasa.
“Maisha ya huku
ni tabu mno basi tu ndio tumezoea. Maji ndio hayo tunanunua na yanapokatika
uende kufuata ziwani kule. Utapandisha ndoo ngapi huku?” alihoji mama huyo
Alisema
alikwisha wahi kusikia kwamba watahamishwa na kupelekwa mahala pengine palipo
bora zaidi lakini hajui mipango hiyo iliishia wapi na wao binafsi hawajawahi
kuulizwa kuhusu hilo.
Sura zinazokinzana
Utayari wa
wakaazi wa milimani wa kuhama makaazi yao ambayo wengine wameishi kwa zaidi ya
miaka 30 kutokana na adha zilizoko unaweza kumfanya mtu kuvunjika moyo na
apoteze hamu ya kuishi milimani.
Kama wewe ni
mmoja wao ni kwa sababu tu haujawahi kutembelea kwenye milima ya Capripoint
Mwanza. Japo kuna ukaribu wa masafa baina ya milima ya ‘Uswahilini’ ya Igogo au
Bugando na milima ya Capripoint tofauti
ya hali ya mazingira na huduma iliyopo baina ya maeneo haya mawili ni kama
ardhi na mbingu ama jehannamu na peponi japo kwa macho utaona kilichotenganisha
milima hiyo ni sehemu ndogo tu ya maji ya Ziwa Victoria.
Kwa mfano wakati katika milima ya
Igogo-Bugando ‘kibarabara’ pekee kilichopo hakiruhusu kuendesha hata baiskeli,
bara bara ya milima ya Capripoint ni pana yenye lami safi, laini na isiyo na
mashimo katika takriban sehemu zake zote.
Kwa upande
mwengine wakati ndani ya makaazi ya milima ya Igogo hakuna hata vichochoro vinavyoruhusu
kubeba jeneza kwa nafasi katika makaazi ya milima ya Capripoint kuna mitaa
mipana iliyoelekea katika kila nyumba ya huko.
Vile vile wakati
nyumba za Milima ya Igogo zikikosa hata mahala pa kuchimba karo za vyoo na maji
machafu nyumba za milima ya Capripoint zina uwanja mpana na wenye kuruhusu
kupanda bustani.
Aidha wakati
kukiwa na tatizo kubwa la maji katika makaazi ya milima ya Igogo, Mahina,
Mkuyuni na Nyegezi na umeme kuonekana tunu kwenye nyumba nyingi katika makaazi
ya milima ya Capripoint maji ni ya ziada kiasi cha mengine kutumika kwa
umwagiliaji bustani.
“Kwa vyovyote
hizi ni sura zinzokinzana na hazileti picha nzuri kuwepo katika eneo
linalokaribiana kama ‘mdomo na pua’ kama ilivyo milima ya Igogo na Capripoint”
alisema Sanjo John nilipomtaka maoni yake baada ya kukamilisha ziara ya Milima
ya Igogo na Capripoint.
Ni kwa
kutembelea milima ya Capripoint tu ndipo mtu anaweza kuona ni kitu gani ambacho
wakaazi wa milima ya Uswahilini (yenye makaazi holela) wanapoteza.
Jambo la kwanza
ambalo ni changamoto kwa wakaazi wa milimani ni usalama wa Afya zao.Kwa kuishi
katika mazingira yasiyo na vyoo vya kutosha, yasiyo na mifumo ya maji taka wala
taka ngumu kama kuna jambo linalowekwa rehani hapo basi ni afya za wakaazi wa
hapo na pengine wa Mwanza kwa jumla.
Afisa wa
maendeleo ya Jamii mkoa wa Mwanza Isaac Ndasa aliliambia gazeti hili kuwa
tatizo la mazingira duni ya wakaazi wa milima ya Mwanza haliwaathiri wao peke yao
bali huwathiri pia walioko bondeni kwa vile uchafu unaozalishwa huko hauishii
huko bali huishia bondeni na pengine kwenye ziwa Victoria.
Jambo la pili
ambalo watu waoishi milima ya Uswahilini wanapoteza na pengine ni changamoto
kubwa kwao na kwa Taifa ni thamani ya ardhi. Kwa mfano wakati Stephano John mkaazi wa Milima ya Capripoint akiniambia kuwa ameahidiwa kiasi cha shilingi 200 milioni na kujengewa
nyumba yenye vyumba vinne iwapo atatoa kiwanja chake kilichopo Capripoint mama
Betrice hana Uhakika hata wa kupata shilingi Milioni 10 iwapo atataka kuuza
nyumba yake iliopo milima ya Igogo.
Jambo la tatu ni
uwezekano wa kupata huduma za mikopo ya kibenki na dhamana. Kwa mfano wakati
wakaazi wa milima ya Capripoint wakiwa na uhakika wa kupata mikopo katika
taasisi yoyote ya kifedha kwa kuweka dhamana ya makaazi yao yaliopo katika
milima hiyo wale wa milima yenye makaazi holelela fursa ya kupata dhamana kama
hiyo ni ndogo mno huko.
Jambo la nne
ambalo watu wanaoishi katika makaazi holela ya milimani wanalikosa ni haki ya
kuishi katika mazingira safi haki ambayo hivi karibuni ilitambuliwa na Umoja wa
mataifa kuwa ni miongoni mwa haki za msingi za kibinaadamu.
Jimmy Luhende
mmoja wa wanaharakati maarufu wa haki za binaadamu Mwanza nilipomuuliza kuhusu
hali ya makaazi holela ya milimani alielezea hali hiyo kuwa ni ya kusikitisha.
Alisema kwamba Uongozi wa jiji la Mwanza ikiwa unashindwa kulishughulikia
tatizo la huko kwa umuhimu wa kuwa na mji uliopangiliwa na wenye kuvutia basi
angalau na walishughulikie tatizo hilo wakijua kwamba mazingira safi ni haki ya wananchi hao ya msingi kama
binaadamu.
Wakati haiba ya
milima ya Capripoint na ile ya Igogo na mingine ya Uswahilini zikikinzana kuna
mkinzano pia juu ya utaratibu wa utoaji wa huduma au usimamizi unaofanywa na
jiji la mwanza katika maeneo haya mawili ambayo yote kimsingi yako chini ya
mamlaka yake.
Mtu anaweza
kujiuliza ni jambo gani lililofanikisha uwepo wa sura nzuri katika milima ya
Capripoint ambalo linashindikana kutekelezwa katika milima mengine ambayo sasa
imegeuka chukizo katika sura ya mwanza. Kwa mtu ataeamua kutembelea maeneo hayo
tofauti kubwa atayoweza kuigundua ni ile ya kipato kwamba wanaoishi milima ya
Capripoint ni Vigogo na wenye nazo wakati wale wa milima ya Igogo na mengine ni
wale ‘waliochoka’. Watu wa pwani huwaita ‘pangu pakavu tia mchuzi’
Hata hivyo
tofauti hiyo haipaswi kuwa kigezo katika utoaji huduma katika nchi kama
Tanzania ambayo katiba yake inatamka wazi wazi kuwa binaadamu wote ni sawa, aliniambia
Kopoka Mlagiri
Nilipoulizia
chanzo cha yote haya alielekeza lawama zake kwa wanasiasa kwamba wanawachochea
watu ama wasihame na waendelee kukaa huko na hulitumia jambo hilo kama ajenda
ya uchaguzi.
Mlagiri alisema
wanasiasa hufikia kuwaambia wakaazi wa huko hasa vijana kwamba wakiwachagua
hawatahamishwa huko milimani na wataendelea kuishi kama kawaida. Alisema
wanasiasa kama hawa ni vigumu kupanga au kutekeleza mpango wowote wa
kuwahamisha watu wa kule. “Si watakosa kura” alisema.
Mkaazi mwengine
wa Mwanza, Abubakar Karsan yeye analaumu mabaraza ya Madiwani. Alisema mara
zote yamekuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kulishinikiza jiji kutekeleza wajibu
wake muhimu hata kama huu wa kushughulikia makaazi holela.
Alisema tatizo hilo ni la muda mrefu na kama ingekuwa Baraza
la madiwani linaubana vyema uongozi wa jiji kutekeleza wajibu wake basi
tatizo lingekwishamalizika zamani.
Ndoto ya Idara
ya Mipango miji ya jiji la Mwanza ni kuwa na mji wenye makazi bora na usio na
migogoro ya ardi lakini ni wakati tu ndio unaoweza kusema iwapo hilo
litawezekana.
MWISHO